Marekani imekataa kutoa visa kwa maafisa kadhaa wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran kabla ya Kombe la Dunia la FIFA la 2026 licha ya majukumu yake kama mmoja wa waandaaji wa tukio hilo la kimataifa.

Ripoti za vyombo vya habari vya Iran na taarifa zilizochapishwa na The New York Times zinasema, ingawa hatimaye Marekani imetoa visa kwa wachezaji wote wa kikosi chenye wachezaji 26 cha Iran, wafanyakazi kadhaa na maafisa wa Shirikisho la Soka la Iran wamezuiwa kuingia Marekani.

Timu ya Taifa ya soka ya Iran maarufu kama Tim Melli ilitarajiwa kuondoka Antalya huko Uturuki kuelekea Tijuana, Mexico, Jumamosi ya leo ili kuendelea na maandalizi ya mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026.

Hata hivyo, maafisa kadhaa walioandamana nao hawajapokea visa ya kuingia Marekani, akiwemo meneja wa timu Mehdi Mohammadnabi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Hedayat Mombeini, Meneja Mtendaji Mehdi Khorrati, meneja wa vyombo vya habari Mohsen Motamedkia, na wanachama wengine wa timu za vyombo vya habari, uchambuzi, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.

Kunyimwa visa maafisa wa timu ya soka ya Iran kunakuja licha ya miezi kadhaa ya uratibu kati ya FIFA na maafisa wa Iran ili kuhakikisha ushiriki wa timu hiyo katika mashindano hayo, ambayo yataandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico.

Kwa mujibu wa The New York Times, zaidi ya wanachama 12 wa wafanyakazi wa usaidizi wa Iran wamenyimwa visa, wakiwemo wakufunzi, wachambuzi na wafanyakazi wa timu ya matibabu. Mehdi Taj, Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, pia amenyimwa visa ya kuingia Marekani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Tasnim, wafanyikazi na maafisa wote wa timu ya taifa ya soka ya Iran wataandamana na timu huko Mexico huku juhudi za kupata visa zao za Marekani zikiendelea.

Iran imepangiwa kucheza mechi zote tatu za hatua ya makundi katika Pwani ya Magharibi ya Marekani, ikianza na New Zealand mjini Los Angeles Juni 15. Timu hiyo pia itamenyana na Ubelgiji mjini Los Angeles na Misri mjini Seattle baadaye mwezi huo.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino na maafisa wakuu wa shirikisho hilo wanaripotiwa kufanya mazungumzo na mamlaka za Iran faraghani katika juhudi za kuzuia kile ambacho baadhi wanakielezea kama mojawapo ya migogoro mikubwa ya kidiplomasia katika historia ya Kombe la Dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *