Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) limechapisha ushuhuda kutoka kwa waandishi wa habari watano wa Kipalestina huko Gaza, ambao walitekwa nyara na askari wa Israel baada ya Oktoba 7, 2023 ikiwa ni pamoja na visa vya unyanyasaji, kuhojiwa na ukiukwaji wa sheria unaohusiana moja kwa moja na shughuli zao za uandishi wa habari.

Waandishi wa habari, ambao ni pamoja na Alaa al-Sarraj, Diaa al-Kahlout, Shadi Abu Sido na Imad al-Ifranji, wameripoti kukumbwa na unyanyasaji mkali, kuhojiwa mara kwa mara kuhusu kazi zao za vyombo vya habari, na unyanyasaji mkubwa wa kimwili na kisaikolojia wakati wa kuzuiliwa kwao na jeshi la Israel.

Akisimulia yaliyompata, Abu Sido amesema kwamba alikamatwa alipokuwa akiripoti habari katika Kituo cha Matibabu cha al-Shifa mnamo Machi 18, 2024, na kwamba amevumilia siku 572 kizuizini, akihamishiwa kati ya magereza ya Sde Teiman, Ofer na Ketziot. Anasema baada ya kuachiliwa alisumbuliwa na matatizo makubwa ya kiafya, kama vile kupoteza uwezo wa kuona katika jicho moja, upele, kifafa, kukosa usingizi na kupoteza hamu ya kula.

Ripoti hiyo ya RSF imefichua kwamba hakuna hata mmoja wa waandishi hao watano wa habari aliyeweza kuendelea na kazi yake baada ya kuachiliwa huru kutokana na athari mbaya za kimwili na kisaikolojia. Sarraj, ambaye alitumia siku 692 katika magereza ya Israel, amesema kwamba amepoteza nyumba yake, gari, vitendea kazi na kumbukumbu ya shirika lake la vyombo vya habari.

Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF) limesema kwamba ushuhuda huo unaangazia kushambuliwa kimakusudi kwa waandishi wa habari wa Palestina kutokana na shughuli zao za kitaaluma, likitaja unyanyasaji huo kama sehemu ya utaratibu wa mateso wa Israel.

Shirika hilo limesisitiza tena takwa lake la kuachiliwa huru haraka waandishi wote wa habari wa Kipalestina wanaoshikiliwa na mamlaka ya Israel, likibainisha kuwa waandishi wa habari 19 wa Kipalestina bado wamefungwa, wakiwemo wawili waliotekwa nyara huko Gaza baada ya Oktoba 7.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *