
Kiongozi wa kanisa katoliki Dunia, Papa Leo XIV amesema uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran haukuwa “vita vya haki”, akisisitiza kwamba itikadi hiyo ya karne nyingi haiendani na uhalisia wa vita vya kisasa.
Papa Leo alitoa matamshi hayo akiwa safarini kwenye ndege ya kuelekea Madrid akitoka Roma jana Jumamosi, ikiwa ni safari ya nne ya kimataifa ya Papa, alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo mgogoro wa Marekani na Israel dhidi ya Iran unaweza kuzingatiwa kama “vita vya haki”, baada ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance kunukuu mafundisho hayo akitetea hatua za kijeshi za Washington dhidi ya Tehran.
“Hakuna vita vya haki hapo,” amesema Papa Leo.
Ameongeza kwamba: “Tatizo ni kwamba nadharia ya vita ya haki inarejea kwenye karne nyingi zilizopita, wakati ambapo watu hawakuweza kufikiria silaha na uwezo wa uharibifu uliopo hii leo.”
Matamshi ya Papa yanakuja huku kukiwa na mvutano baina yake na Rais Donald Trump kuhusu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Tangu kuanza kwa vita hivyo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Leo XIV, amekuwa akitoa wito wa kukomesha uchokozi huo, akionya dhidi ya matamshi ambayo yanaweza kuuchochea zaidi.
Mwezi Aprili mwaka huu pia, Papa Leo alikosoa kauli ya Trump ya kufuta kabisa ustaarabu Iran,” akiitaja kauli hiyo kuwa “haikubaliki kabisa.”
Baadaye Trump alimshambulia Papa akimtaja kuwa ni “dhaifu na mbaya kuhusu sera za kigeni,” matamshi ambayo yaliibua ukosoaji nchini Italia na kumfanya kiongozi huyo wa Vatican aungwe mkono na wanasiasa wengi.
Papa wa Vatican hapo awali alikuwa amesisitiza kuwa: ” Siwezi kuunga mkono vita.” Vilevile Vatican imekemea vikali tabia na sera ya maafisa wa serikali ya Donald Trump ya kutaka kuhusisha vita vya nchi hiyo dhidi ya Iran na imani ya dini ya Kikristo.