
Msemaji wa Jeshi la Yemen ametangaza kwamba kuanzia sasa jeshi hilo limeanza kutekeleza amri ya kupiga marufuku kikamilifu meli zote za utawala haramu wa Israel kupita katika maji ya Bahari ya Shamu au kwa Kiingereza Red Sea na kwamba kuanzia wakati wa kutangazwa marufuku hiyo na kuendelea urambazaji wa baharini wa Israel katika Bahari Nyekundu utakuwa shabaha halali ya jeshi la wanajeshi wa Yemen.
Kauli hii ya “Yahya Saree”, Msemaji wa Jeshi la Yemen, ni tangazo rasmi la kuingia eneo hili katika awamu mpya ya kuzuia hujuma ya adui na hivyo kupanuka eneo la jiografia ya makabiliano na utawala wa Kizayuni hadi katika mojawapo ya njia nyeti zaidi za kistratijia duniani.
Sambamba na jibu la makombora la Iran kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni katika maeneo ya kusini mwa Lebanon na vitongoji vya kusini mwa Beirut, Sanaa pia imejibu uchokozi huo kwa kupiga marufuko meli za utawala huo kupita katika Bahari Nyekundu na Lango-Bahari la Bab al-Mandab na hivyo kuthibitisha kwamba maana ya “Umoja wa Medani” imekuwa kigezo muhimu katika mlingano wa usalama wa eneo.
Kwa mtazamo wa wataalamu wengi wa kieneo na kimataifa, jibu la Iran kwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon limevuka mipaka ya jibu la kawaida la kijeshi. Kwa kushambulia maeneo ya kijeshi ya Israel, Tehran imetuma ujumbe wa wazi kwamba kushambuliwa upande wowote wa mhimili wa muqawama hakutapita bila kulipwa gharama. Umuhimu wa tukio hili unabainika wazi zaidi tunapozingatia kwamba, saa chache tu baada ya Iran kutoa jibu hilo la kijeshi, Yemen nayo ilitangaza rasmi kuingia moja kwa moja kwenye uwanja wa makabiliano.
Kwa hiyo, mojawapo ya njiapanda muhimu zaidi za baharini duniani imekuwa sehemu ya mlingano wa kuzuia hujuma.
Katika miaka ya hivi karibuni, taasisi za kifikra na kiutafiti za Magharibi zimekuwa zikionya juu ya kudhihiri muundo mpya katika mhimili wa muqawama. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, baada ya vita vya Ukanda wa Gaza, ushirikiano kati ya vikosi vya muqawama nchini Iran, Lebanon, Iraq, Yemen na Palestina umeingia katika awamu mpya ambayo inawezesha wanachama wake kuchukua hatua ya wakati mmoja ya kujibu mashambulio katika medani tofauti za vita iwapo mmoja wao atashambuliwa na adui. Matukio ya karibuni yanaonyesha kwamba tathmini hii imekaribia ukweli kwa kiasi kikubwa.
Tangazo la Yemen la kupiga marufuku kupita meli za Israel katika Bahari Nyekundu ni muhimu sana kwa sababu Bab al-Mandab ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za majini kwa biashara ya kimataifa. Njia hii inaunganisha Bahari ya Hindi na Nyekundu na Mfereji wa Suez, ambapo sehemu kubwa ya biashara kati ya Asia, Ulaya, na Afrika hufanyika kupitia njia hii. Kwa hiyo, usumbufu na hitilafu zozote katika eneo hili sio suala la usalama tu kwa utawala wa Israel, bali zinaweza kuwa na madhara makubwa ya kiuchumi na kijiopolitiki kwa dunia nzima.
Vyombo tajika vya habari vya Magharibi vimeelezea mara nyingi kuhusu udhaifu wa kimkakati wa Israel kutokana na masuala ya usalama wa Bahari Nyekundu. Bandari ya Eilat iliyo kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu inategemea sana usalama wa njia ya Bab al-Mandab. Vizuizi vyovyote katika njia hii vinaweza kutoa mashinikizo makubwa ya kiuchumi na kiuchukuzi kwa utawala wa Kizayuni. Kwa sababu hiyo, uamuzi wa karibuni wa Yemen unachukuliwa kuwa chombo muhimu cha kijiopolitiki dhidi ya utawala wa Kizayuni. Wakati huo huo, hatua hiyo ya Yemen ina ujumbe wa wazi kwa Marekani. Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, duru nyingi za kisiasa na kiusalama huko Washington zimedhani kwamba makabiliano yoyote yanayoweza kutokea na Iran au mhimili wa muqawama yanaweza kubanwa ndani ya eneo dogo linalodhibitiwa. Lakini kile kinachoonekana sasa katika eneo ni kinyume kabisa na dhana hiyo. Majibu ya Iran kwa uchokozi wa Wazayuni dhidi ya Lebanon na hatua iliyofuata ya Yemen vinaashiria kwamba katika tukio la vita vikubwa zaidi, wigo wa mzozo huo utavuka mipaka ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kujumuisha maeneo kama vile Bahari Nyekundu, Bab al-Mandab, Ghuba ya Uajemi na hata vituo vya Marekani katika eneo.
Kauli za viongozi wa Ansarullah ya Yemen pia zinatilia mkazo suala hili hili. Wanaamini kwamba matukio ya karibuni yameonyesha kuwa uchokozi wowote mpya dhidi ya Iran au Lebanon hautachukuliwa kuwa ni hatua ndogo tu dhidi ya mhusika maalum, bali utahesabiwa kuwa shambulio dhidi ya mhimili mzima wa muqawama. Hii ndiyo mantiki ileile ambayo imekuwa ikizungumziwa katika miaka ya karibuni chini ya anwani “Umoja wa Medani” na sasa imethibitishwa kivitendo katika uwanja wa vita.
Kuhusiana na hili, jibu la Iran kwa hujuma ya Israel dhidi ya Lebanon na uamuzi wa Yemen wa kuifungia njia ya Bab al-Mandab linapaswa kutathminiwa kama pande mbili za mkakati mmoja ambao unalenga kuongeza gharama za kijeshi, kiuchumi na kisiasa za chokochoko zozote mpya za utawala wa Kizayuni na washirika wake katika eneo. Mkakati mpya unaoanzia Tehran hadi Sanaa, na unatoa ujumbe kwamba zama za kubanwa migogoro katika eneo moja la kijiografia zimepitwa na wakati na kwamba kuchochewa mivutano na ghasia kunaweza pia kuathiri moja kwa moja njiapanda muhimu za biashara na nishati kimataifa. Kwa mantiki hiyo, matukio ya hivi karibuni si sura mpya tu katika makabiliano kati ya mhimili wa mapambano na utawala wa Kizayuni, bali pia ni ishara ya kuibuka mfumo mpya wa kuzuia hujuma ya adui Asia Magharibi, mfumo ambao ndani yake Bab al-Mandab, Bahari Nyekundu, Lebanon, Palestina, na Iran hazichukuliwi tena kuwa medani tofauti, bali ni sehemu za mlingano mmoja wa kimkakati ambao unaweza kubadilisha kabisa mustakabali wa milinganyo ya usalama katika eneo hili.