
Spika wa Bunge la Lebanon amesema kuwa nchi hiyo haitakubali chochote isipokuwa usitishaji vita kamili na usio na masharti kwa upande wa ardhini, anga na baharini, na kusisitiza msimamo thabiti wa Muqawama wa Lebanon dhidi ya hujuma za Israel.
Nabih Berri amesema kuwa majadiliano kuhusu kuondoka kwa wakati mmoja jeshi vamizi la Israel katika ardhi ya Lebanon na wanamapambano wa Hizbullah katika maeneo ya kusini mwa Mto Litan yataanza mara tu baada ya kuanza kutekelezwa usitishaji vita.
Spika wa Bunge la Lebanon pia amepinga kile kinachojulikana kama ” Maeneo ya Majaribio.”
Siyakubali yale yanayotajwa kuwa “Maeneo ya majaribio”. Tunakubali tu kuondoka jeshi la Israel katika maeneo ya kusini na kuingia jeshi la Lebanon katika eneo hilo, na wakati huo huo kurejea nyumbani watu wote waliokimbia makazi yao,” amesema Nabih Berri.
Amesisitiza kuwa Lebanon iko wazi kwa upatanishi wa nchi yoyote kwa lengo la kufikia amani ya kweli.
Wakati huo huo harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetoa jibu kali kwa madai ya uzushi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu kuwasiliana moja kwa moja na harakati hiyo.
Mahmoud Qamati afisa wa ngazi ya juu wa Hizbullah ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya harakati hiyo na Trump, na ameyataja madai hayo ya Washington kama upotoshaji wa kimakusudi unaolenga kujenga taswira ya uwongo kuhusu kufanikiwa katika uga wa diplomasia.
Qamati ameongeza kuwa madai ya Trump ya kupotosha kuhusu kuwasiliana moja kwa moja na Hizbullah yanafichua utayarifu wa Marekani wa kukwepa na kudhoofisha mamlaka husika za Lebanon.