
Harakati ya Hamas imeonya kuhusu ongezeko la shughuli za ubomoaji wa nyumba na majengo ya Wapalestina unaofanywa na Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na al-Khalil, ikitaja vitendo hivyo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati haraka ili kukomesha sera za kuwahamisha Wapalestina kwa mabavu katika makazi na nyumba zao.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imetoa tahadhari kuhusu kampeni hiyo ya “Israel” baada ya matangazo ya hivi karibuni kulenga majengo kadhaa ya makazi na biashara huko al-Khalil.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, harakati hiyo imesema ongezeko hilo linafanana na “vita vya wazi dhidi ya uwepo wa Wapalestina popote pale,” ikiongeza kuwa ubomoaji huo mkubwa unalenga kuwahamisha na kuwang’oa Wapalestina katika ardhi zao kwa mabavu.
Hamas imesisitiza kwamba njama hizo zitashindwa kutokana na kusimama imara kwa Wapalestina, kujitolea kwa ajili ya kutetea haki zao, na Muqawama na mapambano kama njia ya kuelekea kwenye ukombozi.
Taarifa hiyo imekosoa vikali operesheni za ubomoaji wa majengo wa Wapalestina ikiitaja kuwa ni “ukiukwaji mkubwa wa kanuni na sheria zote za kimataifa.” Vilevile imeushutumu utawala vamizi wa Israel kwa kuendelea na sera za kimfumo za “Kuiyahudisha Palestina,” maangamizi ya kizazi na kuwalenga Wapalestina.
Hamas imesema uvamizi na hujuma dhidi ya Ukingo wa Magharibi pia inafanyika sambamba na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel na jitihada za kuwafukuza Wapalestina huko Gaza na al-Quds, na imeihimiza jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kusimamisha shughuli za ubomoaji, kuishinikiza serikali ya Israel na kukomesha uhalifu wa kila siku dhidi ya watu wa Palestina.