
Shirikisho la Soka la Iran limeomba rasmi ruhusa ya FIFA kwa wachezaji wa timu yake ya taifa kuvaa vitambaa vyeusi mikononi wakati wa mechi yao ijayo ya Kombe la Dunia dhidi ya Misri, ili kuenzi mwezi wa Muharram na tukio la Ashura ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS).
Mechi hiyo imepangwa kufanyika Juni 27 huko Seattle, ikiwa ni baada ya Ashura, siku ya kukumbuka mauaji ya Imam Hussein, watu wa familia ya Mtume Muhammad na wafuasi wake mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala nchini Iraq.
Shirikisho la Soka la Iran limesema vitambaa hivyo vyeusi vya mikononi vinakusudiwa kama ishara ya maombolezo na kutoa heshima, na linatarajia FIFA itaidhinisha suala hilo.
Ashura huadhimishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani kote kwa maandamano ya maombolezo, shughuli za kidini na maonyesho ya hadharani ya kudhihirisha huzuni na majonzi kwa mauaji ya watu wa familia ya Mtume Muhammad (SAW).
Ombi la Iran linakuja huku kukiwa na utata unaohusiana na tukio linaloitwa la “fahari” ambalo nchi mwenyeji inataka kuona likifanyika wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya Iran na Misri kwenye mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026.
Mnamo Desemba mwaka jana, Waziri wa Michezo wa Iran, Ahmad Donyamali alithibitisha kwamba Tehran imewasilisha malalamiko rasmi kwa FIFA kuhusu ripoti kwamba manahodha wa timu katika mechi kati ya Iran na Misri watatakiwa kuvaa vitambaa vya mkononi vinavyohusiana na makundi ya watu wanaojihusiaha na maingiliano ya kingono ya jinsia moja (LGBTQ+).
“Hatukubaliani na mtu yeyote linapokuja suala la imani zetu,” alisema Waziri wa Michezo wa Iran.
Iran na Misri zote zilipinga sharti hilo zikilitaja kuwa haliendani na maadili yao ya kidini na kitamaduni, na ziliratibu hatua za pamoja dhidi jambo hilo.
Maafisa wa Iran wametoa wito kwa FIFA kuheshimu maadili ya mataifa yote yanayoshiriki katika mashindano ya Kombe la Dunia.