Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza Jeshi la Polisi Wilaya ya Kigamboni kumkamata Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lingato, Kata ya Kisarawe II, Cosma Kulwa maarufu Kalimanzira, kwa tuhuma za kuuza viwanja mara mbili na kusababisha migogoro ya ardhi kwa wakazi wa eneo hilo.
Agizo hilo limetolewa Juni 11, 2026 wakati wa ziara ya mkuu huyo wa mkoa ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya ya Kigamboni.
Akiwa katika Mtaa wa Kichangani kushughulikia mgogoro wa ardhi unaohusisha zaidi ya familia 23 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), mwananchi mmoja, Hassan, alijitokeza na kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwenyekiti huyo.
Hassan alidai kuwa alinunua eneo la ekari moja kutoka kwa Kalimanzira, lakini baadaye aligundua kuwa eneo hilo lilikuwa limeuzwa kwa mtu mwingine.
Wananchi wengine waliodai kuathirika na mgogoro huo walisema mwenyekiti huyo amekuwa akihusishwa na uuzaji wa viwanja vilivyokuwa na migogoro pamoja na maeneo ambayo tayari yaliuzwa kwa wanunuzi tofauti, hali iliyochangia kuendelea kwa mvutano wa ardhi katika Kisarawe II na maeneo jirani.
Baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi na kushindwa kuwasilisha nyaraka za mauziano, Chalamila aliamuru kukamatwa kwake mara moja na kuwekwa mahabusu hadi kesho.
“Akamatwe na awekewe mahabusu mpaka kesho… kesho atoke mahabusu akiwa na pingu ahudhurie mkutano wa hadhara,” amesema Chalamila.