Akizungumzia vikwazo vilivyowekwa karibuni na Umoja wa Ulaya dhidi ya baadhi ya shakhsia na taasisi za Iran, Kazem Gharibabadi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia Sheria na Masuala ya Kimataifa amesema: ‘Iran haiipi thamani yoyote hatua hiyo ya kimaonyesho ya Ulaya.’

Ameandika katika mtandao wa kijamii wa X: ‘Iran itapuuza hatua hiyo ya Ulaya na kuendelea kutekeleza stratijia yake ya kulinda mamlaka na haki yake ya kusimamia usalama wa Lango-Bahari la Hormuz.

Kaya Kallas, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ambaye ana ushirikiano wa wazi na utawala wa Kizayuni na Marekani, ametoa habari ya kuwekwa vikwazo vipya vya umoja huo dhidi ya Iran.

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena umeibua maswali mazito kuhusu hali ya sera za kigeni za Ulaya, uhuru wa maamuzi yake mbali na Washington na Tel Aviv, na ukweli wa madai yake kuhusu uzingatiaji wa sheria za kimataifa. EU imedai kuwa vikwazo hivyo eti vinalenga kutetea “uhuru wa usafiri wa baharini” katika Lango Bahari la Hormuz. Viongozi wa Ulaya wanadai kwamba hatua za Iran katika lango hilo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa kuhusu safari za meli. Baraza la Umoja wa Ulaya pia limepitisha vikwazo hivyo chini ya mfumo mpya wa kukabiliana na kile linachokiita “vitisho kwa uhuru wa usafiri.” Suala kuu hapa ni kwamba Ulaya leo inadai kutetea uhuru wa usafiri wa majini na sheria za kimataifa, huku katika miezi ya hivi karibuni ikikaa kimya mbele ya mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Wazayuni dhidi ya Iran, ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa, na hata vitisho vya moja kwa moja kwa miundombinu muhimu katika eneo. Huu ndio mkanganyiko uleule unaoashiriwa na wachambuzi wengi wa kimataifa wakiwemo wa nchi za Ulaya yenyewe. Ukweli ni kwamba mgogoro wa Lango Bahari la Hormuz haukutokea katika ombwe. Mgogoro huu ni natija ya moja kwa moja ya kuongezeka mivutano ya kijeshi katika eneo na hujuma za kijeshi za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Hata viongozi wa Ulaya wamekiri mara kwa mara kwamba usalama wa Hormuz unafungamana na matukio ya vita katika eneo. Jambo la kusikitisha ni kwamba, badala ya Umoja wa Ulaya kushughulikia chanzo cha matatizo yaliyopo, umeamua kuyafumbia macho na kuanza kuituhumu Iran kwa njia zisizo za haki.

Mbinu hii inaakisi kiwango cha undumakuwili ambao umekuwa mojawapo ya sababu muhimu za umoja huo kupoteza taratibu itibari yake katika ngazi za kimataifa katika miongo miwili iliyopita. Ulaya inazungumzia umuhimu wa kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa, umoja wa ardhi na sheria za kimataifa kuhusiana na vita vya Ukraine, lakini washirika wake wa Magharibi au utawala wa Kizayuni wanapohusishwa na ukiukaji wa sheria hizo hizo, umuhimu wake hupoteza maana ghafla na kupuuziliwa mbali. Umoja wa Ulaya si mchezaji muadilifu asiyeegemea upande wowote, bali ni sehemu ya kambi yenye nguvu ya Magharibi ambayo hutafsiri sheria za kimataifa kwa maslahi yake yenyewe.

Taasisi za kifikra za Ulaya zimekuwa zikionya katika miaka ya karibuni kuhusu kupungua kwa “nguvu na itibari ya kawaida ya Ulaya ulimwenguni,” itibari ambayo wakati mmoja ilichukuliwa kuwa moja ya thamani zake muhimu zaidi za kimkakati, na sasa imeharibiwa kutokana na sera za undumakuwili za Brussels katika kukabiliana na migogoro ya kimataifa. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Ulaya haiwezi tena kujidhihirisha kama mtetezi wa haki za binadamu na sheria za kimataifa asiye na upendeleo, kwani utendakazi wake unakinzana wazi na madai unayotoa. Hali hii inaonekana wazi katika Lango-Bahari la Hormuz. Umoja wa Ulaya umeiwekea Iran vikwazo kwa kuzingatia tafsiri maalum ya sheria ya usafiri wa baharini, wakati Tehran inasisitiza kuwa si mwanachama wa sheria hiyo na kwamba inatekeleza sheria zake kwa msingi wa sheria zinazokubalika kimatifa na zisizohatarisha usalama wake katika Ghuba ya Uajemi. Gharibabadi amesisitiza kuwa sheria za kimataifa haziwezi kutekelezwa kwa mafanikio kwa kutumia mabavu na kuulazimisha upande mmoja tu uzitekeleze.

Bila shaka vikwazo hivyo vipya vya Ulaya dhidi ya Iran vinakusudiwa kuongeza mashinikizo dhidi ya Tehran na kuimarisha zaidi mikakati ya Marekani katika eneo. Hasa inapotiliwa maanani kwamba sambamba na kutangazwa vikwazo hivyo na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, ametoa wito wa kufanyika mazungumzo mapana kuhusu masuala mengine yanayozozaniwa kati ya Iran na nchi za Magharibi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa vikwazo hivyo havikomei tu katika kadhia ya Hormuz bali ni sehemu ya mashinikizo makubwa zaidi ya kisiasa dhidi ya Tehran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *