Dar es Salaam. Wanawake na wasichana zaidi ya 100,000 nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya kiteknolojia za kidijitali yatakayowawezesha kupata fursa ya kutumia vifaa vya kisasa vya kidijitali, teknolojia zinazoibuka, kushiriki katika ubunifu wa vitendo na kujengewa stadi za kisasa zinazohitajika katika uchumi wa kidijitali.

Mafunzo hayo watayapata katika Kituo cha Ubunifu na Utengenezaji Teknolojia kitakachokuwepo katika Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), ambapo wanawake na wasichana watahama kutoka kuwa watumiaji wa teknolojia pekee na kuwa wabunifu, wavumbuzi na wajasiriamali wa teknolojia katika uzalishaji mali na bunifu mbalimbali.

Hilo linafutatia hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kusaini Makubaliano ya Utekelezaji wa Mradi wa Kituo cha Mabadiliko ya Kidijitali Tanzania DTC, ikiwa ni hatua kuendeleza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kukuza usawa wa kijinsia na mabadiliko ya kidijitali yanayomjumuisha kila mwananchi nchini.

Kupitia makubaliano hayo ya miaka mitatu yanalenga kuimarisha matumizi ya mbinu za kidijitali katika kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi, sambamba na kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu na kunufaika na ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Akizungumza Alhamisi, Juni 11, 2026 jijini Dar es Salaam katika halfa ya utiaji saini, Mkurugenzi wa Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Badru Abdunuru amesema lengo ni kuwafikia wanawake 100,000 kupitia mradi huo wa miaka mitatu ya awali ingawa inaweza kufikiwa wanawake wengi zaidi.

“Mradi unataka kuimarisha ushiriki wa wanawake na wasichana kwenye uchumi wa kidijitali ili kuongeza ushiriki wao kupitia mafunzo mahususi yatakayopatikana Shirika la TIRDO ya namna ya kutumia teknolojia hizo,” amesema.

Amesema kituo hicho kitakuwa na zana zote za kujifunzia namna ya kutumia teknolojia katika uzalishaji wao na mafunzo pia yatapatikana katika vituo vya chuo cha maendeleo ya jamii, na Tengeru.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi mkaazi wa GIZ Tanzania, Anne Hahn amesema ushirikiano huu tayari ulishaanza kuzaa matunda kabla hata ya utiaji saini wa makubaliano rasmi.

“Kupitia ushirikiano na Shirika la TIRDO, GIZ inasaidia kuanzisha maabara ya kidijitali na karakana ya ubunifu maalum kwa ajili ya wanawake na wasichana ili kuwageuza kuwa wabunifu na wajasiriamali,’’ amesema.

Marlene Landes, Kaimu Mkuu wa Ushirikiano ubalozi wa Ujerumani amesema utiaji saini unaonyesha nia ya pamoja ya kuhakikisha mabadiliko ya kidijitali yanatoa fursa kwa kila mtu bila kuacha mtu nyuma.

Amesema teknolojia inapaswa kutumika kwa uwajibikaji ili kukuza uhuru wa kujieleza, kupata taarifa, na uwezeshaji wa kiuchumi.

Kwa upande wake Mhandisi Esther Lazaro kutoka TIRDO, amesema kupitia mradi huo wanawake na wasichana watageuza mawazo yao kuwa bidhaa kupitia msaada wa kidijitali utakaotolewa na kituo hicho.

“Tutafanya watatue matatizo yanayowakabili wanawake na Tanzania kwa ujumla kupitia vifaa na mafunzo watakayoyapata,” amesema.

Mradi    huo unaendana na vipaumbele vya maendeleo vya taifa vilivyobainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake ya Mwaka 2023, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Mwaka 2024–2034.

Aidha, GIZ kwa kushirikiana na Tanzania inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Maabara ya Ubunifu wa Kidijitali (Digital Fabrication Lab).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *