
Dar es Salaam. Yanga imeendeleza ubabe wake kwa Mashujaa FC baada ya leo Jumamosi, Juni 13, 2026 kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Ushindi huo wa Yanga leo umeifanya ifikishe pointi 63 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi.
Mabao ya ushindi ya Yanga leo yamefungwa na kiungo Mudathir Yahya na beki Bakari Mwamnyeto.
Mudathir amefunga bao la kwanza katika dakika ya 28 akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kulia, pasi ya kichwa ya Prince Dube.
Bao lingine la Yanga limepachikwa katika dakika za lala salama na nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto aliyemalizia mpira uliochelewa kuokolewa na walinzi wa Mashujaa FC baada ya shambulio la Maxi Nzengeli.
Yanga sasa inahitaji kuvuna pointi 11 katika mechi nne ilizobakiza ili ijihakikishie taji la Ligi Kuu msimu huu.
Kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Mbeya City waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mfungaji akiwa ni Adili Buha.
Matokeo hayo yameifanya Mbeya City kufikisha pointi 25 huku ikiendelea kubakia katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.