MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube bado hajasaini mkataba mpya Yanga, jambo ambalo linaongeza presha kwa wanajangwani hao, huku vigogo wa Afrika Kusini, Kaizer Chiefs ikikazia kutokana na kuhitaji saini ya Mzimbabwe huyo.

Ni hivi. Dube ambaye amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga katika misimu miwili iliyopita bado hajatia saini mkataba mpya licha ya mazungumzo kati ya pande hizo kuanza tangu dirisha dogo msimu huu.

Mzimbabwe huyo amekuwa miongoni mwa washambuliaji waliotoa mchango mkubwa Yanga tangu alipojiunga na klabu hiyo.

Katika kipindi cha misimu miwili akiwa Jangwani, amekuwa mhimili wa safu ya ushambuliaji kwa kufunga mabao muhimu kwenye mashindano mbalimbali na kusaidia timu hiyo kuendelea kutawala soka la ndani.

Uwezo wake wa kutumia nafasi, nguvu katika kushambulia na kutengeneza nafasi kwa wenzake umemfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotazamwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara, huku akifunga mabao 22 ndani ya misimu miwili ingawa bado ana mechi nne za kumaliza msimu.

KAIZER YAIPA UGUMU YANGA

Taarifa za ndani zilieleza ofa hiyo ya Kaizer Chiefs ndiyo inayosababisha mshambuliaji huyo kuchelewesha hatua ya mwisho ya kuweka saini yake, huku Yanga ikiwa tayari haijafahamu uwepo wa dili hilo kutoka Afrika Kusini.

Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa alithibitisha klabu hiyo inaendelea na mazungumzo na Dube, lakini haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa mchezaji huyo kama ana ofa nyingine.

“Dube bado hajasaini mkataba lakini mazungumzo yetu tulianza vizuri na tupo vizuri ingawa bado hajamaliza kuweka saini yake. Hizo taarifa ana ofa Afrika Kusini tumezisikia muda mrefu ingawa mwenyewe bado hajatuletea.”

Aliongeza Kaizer Chiefs si mara ya kwanza kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo kwani ilishawahi kuwasiliana na Yanga hapo nyuma lakini klabu hiyo ilikataa kumuuza kutokana na umuhimu wake kwenye kikosi.

“Tunafahamu Kaizer Chiefs ilikuwa inamtaka muda mrefu, ilishawahi hata kuja kwetu huko nyuma lakini tulikataa kumuuza. Bado ni mchezaji ambaye tunahitaji abaki hapa,” alisema.

Yanga imeweka wazi haitaki kumpoteza Dube na tayari imemwandalia ofa kubwa ambayo inaamini inaweza kumshawishi kuendelea kubaki Tanzania badala ya kuhamia Afrika Kusini.

“Tumeendelea naye kwa sababu tunamtaka na tutaendelea kufanya hivyo ili tumalizane, lakini mwenye maamuzi ya mwisho ni mchezaji mwenyewe,” aliongeza kiongozi huyo.

MSALA UPO KWA DUBE

Kwa sasa presha ipo kwa Dube ambaye anatakiwa kufanya maamuzi kati ya kuendelea na maisha yake ndani ya Yanga ambako amepata mafanikio, au kujaribu changamoto mpya kwenye soka la Afrika Kusini.

Kabla ya kutua Yanga Dube alikuwa miongoni mwa mastaa ambao hawakuweza kuficha hisia za mapenzi yake juu ya timu hiyo, kwani wakati yuko Azam aliwahi kuonekana mara kadhaa uwanjani akienda kuitazama ilipokuwa ikicheza, huenda ataamua kusalia kutokana na mapenzi hayo au ataondoka kufuata maslahi.

NAFASI ANAYO SAUZI

Kwa kuangalia ishu ya nafasi ndani ya kikosi cha Kaizer, Dube anayo kwani mchezaji kinara wa eneo hilo Flavio Silva anarekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mechi 22 alizocheza.

Huku Makabi Lilepo Mkongomani anayechezea timu hiyo katika nafasi ya winga na mshambuliaji akiwa na mabao 05 kwenye mechi 27, Wandile Duba akiwa nayo matatu. Hivyo kwa upande wa rekodi Dube bado ni mwamba ukilinganisha na washambuliaji walioko ndani ya klabu ya Kaizer, kwani hakuna aliyemfikia.

Kingine ambacho kinaweza kuwa sababu ya Dube kusalia Yanga ni nafasi na rekodi kwenye msimamo, ukilinganisha na Wasauzi hao ambao wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa wamemaliza na pointi 54, ilhali Yanga ikiwa ndiye bingwa mtetezi wa Kombe la Ligi Kuu Bara, ikichukua mara nne mfululizo, mpaka sasa inapoiti 60 kwenye mechi 25 ilizocheza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *