
Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati limekanusha taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna njama ya kutaka kuipindua serikali, na kusisitiza kuwa nchi hiyo ina utulivu wa kutosha, na kwamba taasisi za serikali zinafanya kazi kama kawaida.
Katika taarifa nadra kutolewa kwa umma, Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati amepuuza madai ya kuwepo jaribio la mapinduzi na kusema taarifa hizo hazina ukweli wowote.
Amesema upotoshaji huo unalenga kuibua mkanganyiko na kudhoofisha imani ya umma. Maafisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamewataka waanchi kutoshawishiwa na uvumi; na badala yake wategemee tu vyanzo rasmi vya habari.
Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati limekanusha taarifa kuhusu njama ya mapinduzi huku nchi kadhaa za Kiafrika katika miaka ya karibuni zikiwa zimeshuhudiwa mapinduzi ya kijeshi. Kwa hiyo, ripoti ambazo hazijathibitishwa za ukosefu wa utulivu wa kisiasa mara nyingi huenea haraka mtandaoni.
Mamalka husika huko Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zimeeleza kuwa askari usalama wanaendelea na shughuli zake kikamilifu na wamesalia watiifu kwa serikali ya Rais wa nchi hiyo Faustin- Archange Touadera. Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati pia limeonya kuhusu kusambaza habari zozote za uwongo likisema kuwa ripoti kama hizo zinaweza kutishia usalama wa taifa na utulivu wa umma.
Taarifa hii imelenga kuwatoa hofu wananchi na washirika wa kimataifa wakati huu ambapo Jamhuri ya Afrika ya Kati inaendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama licha ya juhudi za kuleta utulivu nchini humo.