#HABARI: Jeshi la Polisi Nchini Tanzania kupitia kwa Msemaji wake Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime limesema linafuatilia kwa karibu wale wote wanaohamasisha matukio ya uvunjifu wa amani Nchini kupitia mitandao ya kijamii.
Kulingana na Kamanda Misime katika taarifa yake ya leo Ijumaa Juni 19, 2026, watu hao pia wamekuwa wakidiriki kutumia mitandao ya kijamii kuhamasishana kuvamia askari wa Vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwapora silaha ili kuzitumia kufanya uhalifu wanaoupanga kuufanya Nchini.
Polisi imesisitiza kwamba hakuna haki ya kuhamasisha kufanya vitendo vya uhalifu kama vinavyokusudiwa kuhatarisha usalama wa maisha ya watu na mali zao na vinavyokiuka haki za watu wengine kwa kuwajengea hofu kila siku na kutaka kuwanyima uhuru wao wa kufanya shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato.
Kamanda Misime kadhalika ametoa wito kwa wananchi wote kwa umoja wao kuendelea kushirikiana katika kukataa na kupinga vitendo vyote vya kihalifu vinavyolenga kuhatarisha maisha ya wananchi, mali zao na mali za umma na amani ya Nchi, Polisi ikimtaka kila mmoja atakayepokea ujumbe wa hamasa ya kushiriki kwenye uhalifu kutousambaza ujumbe huo na badala yake waufute na kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili hatua zichukuliwe.
(Feed generated with FetchRSS)