Dar es Salaam. Oya! zile pisi zilizoteka jukwaa la Diamond Jubilee. ‘Taim’ ambayo Baharia wa Msoga katia kambi rasmi Ikulu ya Magogoni? 2006 hiyo ‘Misi Tizedi’ ya moto sana. Hapa Wema, pale Jokate, kule Lisa huku Irene. Achana na Anti aliyeshika nafasi za Everton.
Kuna ‘Topu Faivu’ na ‘Topu Teni’. Kuanzia namba 6 kurudi nyuma ndo na Anti alikuwepo. Ni mwaka wa kipekee uliotuzalishia mastaa wa kipekee. Leo ni mashangazi wote lakini majina yao bado yapo juu kama mbalamwezi. Kimsingi bado ‘brandi’ zao zina hadhi ya nyota tano.
Kati ya wale ‘Mamisi’ wa 2006 ni Wema, Jokate, Uwoya na Anti na kidoogo Lissa. Ambao walibaki ‘meinstriim’ na kugeuka mastaa nje ya ‘umisi’ wao. Uigizaji filamu kikawa kiwanda cha ‘kumeintein’ ustaa wao. Tulisahau hata kama walikuwa ‘mamisi’ hapo kabla.
Katika hao watano, akaongezeka Jack Wolper. Huyu Mkibosho au Mmarangu hakuwahi kuwa ‘Misi’, alikuwa winga tu kitaa huko. Na yeye aliona magazetini sura na majina ya kina Wema. ‘Mara pap’ akajikuta katikati yao kwa kupitia sanaa ya uigizaji. Wakawa timu moja hatari.
Hii timu ya madem hawa wakali wa mjini. Ilivuka malengo ya timu ya madem wakali wa mjini wale wa kabla yao. Naongelea timu ya Al Qaeda iliyoongozwa na Amina Chifupa (rest ize sis’), Sinta, Nora na Maimartha wa Jesse. Timu hii imekutana na mitandao.
Kina Amina waliteka kurasa za magazeti ya Udaku. Kina Wema waliteka magazeti ya udaku. Na wakateka kurasa za mitandaoni. Ustaa wao umedumu kwa miaka mingi. ‘Twenti yiazi mai frendi’ ni wao tu kwenye ‘kategori’ zote za ustaa wa mastaa wa kike.
Alianza Uwoya miaka mingi ‘baki in dei’. Akajiweka jumla jumla kwa ‘futibola’ kutoka kwa Paulo hapo jirani. Ndikumana Katauti (‘resti ize bro’), alimuhusudu dada yetu mpaka siafu na kumbikumbi za Ubena Zomozi zilitambua hilo. Irene alipendwa kinoma babu, ule upendo wa Agape.
St. Joseph, kanisa lililotumika kuwabariki na kuwa ‘wani bode’. Mazonge yakatokea ila mwamba aliacha mbegu. Irene akawa staa wa kwanza uzao wa Mis Tz 2006 kujifungua. Ilikuwa ni kama utani ‘supa staa gredi wani’ kusitisha bata za mjini na kuishi kindoa.
Hadi sasa anaweza kuwa ndiye staa aliyeishi kistaa ndani ya ndoa. Kila mwezi ungemuona ‘temino wani’ anapaa au kutua kutoka ‘Saiprasi’. Akimfuata ‘hazibandi’ aliyekuwa anapiga mbugi la kulipwa huko. Kamera za udaku ziliteseka sana.
Ilipita miaka mingi sana kabla ya Anti kumjibu. Baada ya kumzalia dansa wa ‘Mondi’ Mose Iyobo. Na baada ya hapo Jack Wolper naye akashusha injini za fasta fasta. Jokate naye akaona siyo kesi akashusha injini. Huyu ni juzi kati tu hapo. Akabaki kubwa lao.
Kibinaadam utaelewa mawazo ya Wema kwa kipindi chote hichi. Irene fresh, Anti mzuka, Wolper oya oya, Jokate woyoo. Wema tu. Tunaweza kusema alijikondesha kumbe alikondeshwa na mawazo tele. Hata furaha yale na machozi ya Anti, yanatoa picha ya nyuma ya pazia.
Kelele zilikuwa nyingi na bahati mbaya au nzuri. Wema anavutia kunangwa, kusemwa, kutetwa na kusengenywa. Kuanzia mitandao hadi mitaani, Wema kakaa katika vinywa vya watu utadhani ndiye aliyewanyima wote utajiri.
Watu sampuli yake wapo dunia nzima. Kuna watu ni ‘stori meka’ toka tumboni mwa mama zao. Ni kama Wema ama Diamond vile, hawa ni ‘nyuzi meka’ na hawajali. Tazama pamoja na kujifungua bado anasemwa kwamba kafeki.
Walimsema kwa kutozaa na sasa wanamsema kwa kuzaa. Na tena watasema kwa kulea. Uzuri wake dunia ya sasa kadiri unavyotajwa na kuandikwa sana, ndivyo pesa inavyoingia.
Wema ni ‘brand’ tena siyo ndogo, ni ‘brand’ inayoweza kugeuza buluu kuwa njano fasta.
Kama huamini, siku zinasambaa taarifa za kujifungua kwake. Kule Marekani kombe la dunia lilikuwa tayari. Lakini Wema ‘katrendi’ ile sana tu kitaani, mitandaoni kila kona Wema. Stori za ‘Wodi Kapu’ hazijazuia ‘trendi’ ya toto la taifa kusambaa kama habari za Mnara wa Mlinzi.
‘Dream Team’ ya Wema, Jokate, Uwoya, Anti na Wolper. Alibakia Wema peke yake kuitwa mama. Hawa kwa sasa ‘era’ yao imefika kikoma. Ni wazazi ndo wasaa wa kulea watoto ili waje kuwa kama wao kwa ustaa na siyo kwa tabia.
Ni rahisi Wema kumueleza mtoto wake madhara na faida ya ustaa. Ni rahisi Irene kumuongoza Krish ili awe staa bila changamoto za maumivu. Ni rahisi Anti au Wolper kumuepusha mtoto na athari za ustaa. Akapita njia bora ya ustaa.
Mtoto wa Taifa ni mchanganyiko wa Zanzibar, Singida, Marangu Mtoni kama siyo Kiboriloni na Sinza Mori. Wema ni jibu kamili kuwa usikate tamaa chini ya jua. Kwa wale ambao hawajabarikiwa watoto mpaka leo. Ipo siku yenu.