Washington. Rais Donald Trump amezindua rasmi ndege mpya ya Rais wa Marekani, Air Force One, ambayo awali ilikuwa mali ya familia ya kifalme ya Qatar, kabla ya kutolewa kama zawadi kwa Serikali ya Marekani.
Ndege hiyo aina ya Boeing 747-8 imeelezwa kuwa moja ya ndege za kifahari zaidi kuwahi kutengenezwa duniani, ikiwa na thamani inayokadiriwa kufikia dola 400 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1 trilioni).
“Ndege hii imegeuzwa kuwa Ikulu inayoruka angani au ‘kasri la angani’, yenye kiwango cha anasa ambacho hakijawahi kuonekana popote duniani,” alisema Trump wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jana Ijumaa katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Andrews, ikishuhudiwa na mamia ya askari wa Jeshi la Anga la Marekani.
Trump alitoa kauli hiyo baada ya kushuka kwenye ndege hiyo huku wimbo wake maarufu wa kampeni, ‘God Bless the USA’ (Mungu ibariki Marekani), ukipigwa.
Rais huyo pia alithibitisha kuwa ataitumia ndege hiyo katika safari yake ya mkutano wa Nato utakaofanyika Ankara, Uturuki mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Trump, safari yake ya kurejea kutoka mkutano wa Kundi la G-7 nchini Ufaransa wiki hii, ndiyo ilikuwa ya mwisho iliyopangwa kutumia Air Force One ya zamani.
“Kuanzia sasa, tutakapotua katika viwanja vya ndege vya London, Ujerumani na sehemu nyingine duniani, hakuna ndege itakayoweza kuizidi hii. Hivyo ndivyo taifa letu linavyopaswa kuwakilishwa,” alisema Trump.
Ndege mbili za zamani aina ya Boeing 747 zinazotumiwa katika msafara wa rais wa Marekani ziliingizwa rasmi katika huduma mwaka 1990 wakati wa utawala wa Rais George H.W. Bush.
Mapema mwaka huu, moja ya ndege hizo ililazimika kurejea Washington wakati wa safari ya Rais Trump kwenda Davos, Uswisi, baada ya kubainika hitilafu ya kiufundi ikiwa safarini.
Katibu wa Habari wa Ikulu, Karoline Leavitt alisema wahudumu wa ndege waligundua tatizo dogo la mfumo wa umeme na kuamua irudi katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Andrews kwa tahadhari, hali iliyosababisha hata Rais Trump kuchelewa kuwasili Davos.
Ndege iliyozinduliwa itatumika kama ndege ya mpito, au “bridge aircraft”, kumhudumia Rais wa Marekani hadi pale ndege mbili mpya za rais zilizotengenezwa maalumu na kampuni ya Boeing, zitakapokamilika na kukabidhiwa mwaka 2028.
Ikulu inayoruka angani
Wataalamu wa anga wanaielezea ndege hiyo kama “Ikulu inayoruka angani” kwa sababu ina uwezo wa kumwezesha Rais kuendelea kutekeleza majukumu yake akiwa safarini.
Ndani ya ndege kuna ofisi kamili ya Rais yenye mifumo ya mawasiliano ya siri, inayomwezesha kuwasiliana moja kwa moja na viongozi wa dunia, makamanda wa kijeshi na taasisi mbalimbali za usalama.
Vyumba vya kulala, starehe za kifalme
Moja ya sifa zilizovutia wengi ni kiwango cha anasa kilichomo ndani ya ndege hiyo. Kabla ya kufanyiwa marekebisho ya kijeshi, ndege hiyo ilikuwa imeundwa kwa ajili ya familia ya kifalme ya Qatar na ilikuwa na vyumba vitatu vya kulala vya kifahari, sebule binafsi, ofisi na maeneo maalumu ya kupumzikia.
Mwonekano wa ndani wa ndege mpya ya Rais wa Marekani, Air Force One.
Maumbo ya ndani yamehifadhiwa kwa kiwango kikubwa, huku sakafu, mbao za thamani, viti vya ngozi na mapambo ya hali ya juu yakibaki sehemu ya muonekano wake.
Rais Trump mwenyewe alisema ubora wa vifaa vilivyotumika ndani ya ndege hiyo ni wa kiwango cha juu kiasi kwamba “ni vigumu kuamini macho yako unapoviona.”
Ndani ya ndege pia kuna vyumba vya wageni wa ngazi za juu, maeneo ya chakula, mabafu ya kisasa na maeneo ya kupokea wageni wa kimataifa.
Ukumbi wa mikutano angani
Kwa kuwa Rais wa Marekani anahitaji kufanya maamuzi muhimu muda wote, ndege hiyo imewekewa ukumbi maalumu wa mikutano unaoweza kutumiwa kufanya vikao vya usalama wa taifa, mikutano na washauri wakuu au mazungumzo ya kidiplomasia.
Ukumbi huo umeunganishwa na mifumo ya mawasiliano ya satelaiti inayowezesha mikutano ya video na mawasiliano ya moja kwa moja kutoka popote duniani. Hii ina maana kwamba hata akiwa katikati ya Bahari ya Atlantiki au Pasifiki, Rais anaweza kuendesha shughuli za Serikali bila usumbufu.
Usalama wa juu
Ingawa ndege hiyo ilianza kama ndege ya kifahari ya kiraia, Jeshi la Anga la Marekani limeifanyia maboresho makubwa ya kiusalama kabla ya kuikabidhi kwa matumizi ya Rais.
Rais wa Marekani, Donald Trump akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege mpya ya Rais ya Air Force One aina ya Boeing 747-8.
Kwa mujibu wa Jeshi la Anga, mifumo yote ya mawasiliano, vifaa vya usalama, ulinzi dhidi ya mashambulizi ya kielektroniki na teknolojia za siri vimeboreshwa.
Serikali ya Marekani imesema vitisho vyovyote vilivyoweza kuwepo kutokana na umiliki wake wa awali “vimeondolewa kabisa”.
Ndege hiyo ina uwezo wa kuhimili mazingira magumu ya kiusalama, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kielektroniki, udukuzi wa mawasiliano na vitisho vingine vinavyoweza kutokea wakati wa safari za Rais.
Kama ilivyo kwa Air Force One nyingine, ndege hii pia inaweza kuendelea kufanya kazi hata katika nyakati za dharura za kitaifa. Mfumo wake wa mawasiliano umeundwa kuhakikisha rRais anabaki kuongoza taifa hata kama kutatokea mgogoro mkubwa wa kijeshi au kiusalama.
Kasi, uwezo wa kuruka mbali
Boeing 747-8 ni moja ya ndege za abiria zenye kasi kubwa zaidi duniani. Ina uwezo wa kusafiri kwa kasi ya takribani kilomita 988 kwa saa katika safari za kawaida.
Ndege hiyo inaweza kuruka umbali wa zaidi ya kilomita 14,000 bila kujaza mafuta. Hii inamaanisha inaweza kusafiri kutoka Washington kwenda Mashariki ya Kati, Ulaya au Asia kwa safari moja bila kutua njiani.
Inatumia injini nne za kisasa aina ya General Electric GEnx ambazo zinatajwa kuwa miongoni mwa injini bora zaidi za ndege duniani kwa ufanisi wa mafuta, nguvu na utulivu wa safari.
Licha ya anasa na uwezo wake mkubwa, ndege hii haitakuwa ya kudumu, itatumika kama suluhisho la muda wakati Marekani ikisubiri ndege mbili mpya za VC-25B zinazotengenezwa na Boeing.
Mwonekano wa ndege mpya ya Rais wa Marekani, Air Force One aina ya Boeing 747-8.
Mradi huo umekumbwa na ucheleweshaji mkubwa na ongezeko la gharama, jambo lililosababisha Serikali kutafuta njia mbadala ya muda.
Wakosoaji wanaona hatari
Licha ya sifa hizo, zawadi hiyo imezua ukosoaji mkali kutoka kwa wanasiasa wa vyama vyote viwili nchini Marekani.
Wakosoaji wanahoji kwa nini Marekani, taifa lenye uchumi mkubwa duniani, likubali zawadi ya ndege ya mamia ya mamilioni ya dola kutoka kwa serikali ya kigeni.
Baadhi ya wabunge wa Chama cha Democratic wameeleza kuwa hatua hiyo inaweza kukinzana na Katiba ya Marekani inayowazuia viongozi wa serikali kupokea zawadi kutoka kwa mataifa ya nje bila idhini ya Bunge.
Seneta Adam Schiff ni miongoni mwa waliohoji uhalali wa mpango huo, akisema kipengele cha Katiba kinazuia viongozi kupokea “zawadi yoyote” kutoka kwa watawala wa kigeni bila ruhusa ya Congress.
Mbali na wapinzani wa kisiasa, baadhi ya wafuasi wa Trump pia wameonyesha wasiwasi.
Mchambuzi maarufu wa kihafidhina, Ben Shapiro alihoji sababu za Qatar kutoa ndege hiyo ya thamani kubwa, akisema hakuna taifa linalotoa zawadi ya aina hiyo bila kuwa na masilahi fulani.
Mwanaharakati wa mrengo wa kulia Laura Loomer, ambaye mara nyingi humtetea Trump, alisema mpango huo unaweza kuwa doa katika utawala wa rais huyo.
Gazeti la New York Post, ambalo mara nyingi huunga mkono sera za kihafidhina, lilichapisha tahariri likisema ndege hiyo si “zawadi ya bure” kama inavyowasilishwa.
Qatar Yajibu
Serikali ya Qatar imekanusha madai kuwa zawadi hiyo inalenga kununua ushawishi nchini Marekani.
Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, amesema makubaliano hayo ni ya serikali kwa serikali kupitia wizara za ulinzi za nchi hizo mbili.
Mwonekano wa ndani wa ndege mpya ya Rais wa Marekani, Air Force One.
“Kwa nini tununue ushawishi nchini Marekani? Qatar imekuwa mshirika wa kuaminika wa Marekani kwa muda mrefu,” alisema.
Kwa upande wake, Trump amesisitiza kuwa ndege hiyo haitakuwa mali yake binafsi na kwamba baada ya kumaliza muda wake wa urais itawekwa katika maktaba yake ya urais kama sehemu ya historia.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.