
Kiungo wa Uturuki, Arda Guler amewaomba radhi mashabiki wao kufuatia kuondolewa mapema kwa timu yao ya taifa katika Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea Mexico, Marekani na Canada.
Kichapo cha bao 1-0 ambacho Uturuki imekipata kutoka kwa Paraguay, usiku wa kuamkia leo kwa muda wa Afrika Mashariki, kinamaanisha kwamba timu hiyo itashuika mkia kwenye kundi D hata ikipata ushindi katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Marekani, jambo linaloifanya isubirie kukamilisha ratiba tu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Guler anayeichezea Real Madrid amesema kuwa wao kama wachezaji wanastahili kubeba lawama kutokana na aibu hiyo waliyokumbana nayo.
Guler amesema kuwa kiwango walichoonyesha katika fainali hizo, hakiendani na kariba za wachezaji wanaounda kikosi cha Uturuki.
“Tunaomba msamaha na tunajisikia aibu. Wote tunacheza katika klabu kubwa na tulitakiwa kufanya vizuri zaidi katika haya mashindano. Katika mechi mbili hatujafunga bao na hili halikubaliki,” amesema Guloer.
Uturuki imekuwa timu ya pili kuondolewa katika mashindano hayo, ikitanguliwa na Haiti ambayo ilipokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brazil.
Hii ni mara ya pili kwa timu ya Taifa ya Uturuki kuondolewa katika hatua ya makundi kwenye Fainali za Kombe la Dunia katika mara tatu ilizowahi kushiriki.
Mara ya kwanza ilikuwa ni 1954 wakati mashindano hayo yalipofanyika Switzerland.
Hata hivyo mwaka 2002, Uturuki ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu wakati fainali hizo zilipofanyika Korea na Japan.