
Dar es Salaam. Wakati Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiendelea kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliosababisha vifo vya watu 232, matumaini mapya yanaibuka katika ulimwengu wa sayansi baada ya wataalamu wa Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza, kuanza kutumia Akili Unde (AI) kubuni chanjo za kizazi kipya zinazolenga kupambana na Ebola na magonjwa mengine ya virusi.
Hatua hiyo inakuja huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likiripoti kuwa hadi Juni 19, 2026, watu 896 walikuwa wameambukizwa Ebola nchini Congo, huku 232 wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa mlipuko huo umeongeza umuhimu wa kuharakisha tafiti za kisayansi zinazoweza kusaidia kupata chanjo zenye uwezo mkubwa zaidi wa kuzuia magonjwa hatari ya kuambukiza, hususan yale yanayosababishwa na virusi vinavyobadilika mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Chanjo (Gavi the Vaccine Alliance), timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge mbali ya ugonjwa wa Ebola, tayari imefanikiwa kutengeneza chanjo ya kwanza ya Uviko-19 ambayo pia ilibuniwa kwa kutumia Akili Unde na ambayo imefikia hatua ya majaribio kwa binadamu.
Chanjo hiyo ya majaribio imelenga kuuchochea mfumo wa kinga ya mwili kuzalisha kingamwili zinazoweza kutambua aina mbalimbali za virusi vya Uviko-19.
Matokeo ya awali yanaonyesha chanjo hiyo ilikuwa salama kwa washiriki wa utafiti, ingawa kiwango cha mwitikio wa kinga kilikuwa cha wastani.
Mbali na chanjo ya Ebola na Uviko-19, watafiti hao wanaendelea kufanya tafiti nyingine zinazohusisha chanjo za mafua ya msimu ambazo zinaweza kutumika kwa muda mrefu bila kuhitaji kubadilishwa kila mwaka.
Pia, wanafanyia kazi chanjo dhidi ya mafua ya ndege aina ya H5N1, ambayo wataalamu wengi duniani wanaendelea kuyafuatilia kutokana na hatari yake ya kusababisha milipuko mikubwa ya magonjwa.
Akizungumzia hatua hiyo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Alex Msoka amesema kufanikiwa kufikisha chanjo iliyobuniwa kwa kutumia AI katika hatua ya majaribio ya binadamu ni mafanikio makubwa katika sayansi ya tiba.
Amesema mchakato wa kutengeneza chanjo hupitia hatua nyingi muhimu ikiwemo tafiti za maabara, majaribio kwa wanyama na baadaye kwa binadamu, hivyo kufikia hatua ya majaribio ya binadamu ni ishara kwamba utafiti huo umefikia kiwango cha juu cha maendeleo.
“Moja ya faida kubwa za matumizi ya Akili Unde ni uwezo wake wa kuchambua kwa haraka taarifa nyingi za kisayansi na kubaini kwa usahihi aina za virusi vinavyolengwa. Hii inaweza kusaidia kubuni chanjo zenye ufanisi mkubwa zaidi,” amesema Dk Msoka.
Kwa mujibu wake, matumizi ya AI yanaweza kufungua ukurasa mpya katika maendeleo ya chanjo duniani kutokana na uwezo wake wa kubuni kinga zinazolenga aina maalumu za virusi kwa usahihi mkubwa.
“Hata Ebola ina aina tofauti za virusi. Teknolojia ya AI inaweza kusaidia kutengeneza chanjo zinazolenga aina husika kwa ufanisi zaidi kuliko baadhi ya mbinu zinazotumika sasa,” amesema.
Aidha, Dk Msoka anaamini kuwa katika miaka michache ijayo, matumizi ya Akili Unde yatachangia kuharakisha kwa kiasi kikubwa tafiti za chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayoendelea kuwa tishio kwa afya ya binadamu.
Hata hivyo, wataalamu wengine wanasisitiza umuhimu wa kuendelea kufuata taratibu zote za kisayansi kabla ya chanjo yoyote kuruhusiwa kutumika kwa umma.
Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema matumizi ya AI ni hatua nzuri katika maendeleo ya teknolojia ya afya, lakini hayaondoi umuhimu wa kufuata hatua zote zinazotakiwa katika utafiti wa chanjo.
“Teknolojia inaweza kusaidia kuharakisha baadhi ya hatua za utafiti, lakini bado lazima kuwe na majaribio ya maabara, tathmini za usalama na uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika kabla ya chanjo kuanza kutumika,” amesema.
Amesema pamoja na maendeleo ya kisayansi yanayoendelea kushuhudiwa duniani, kinga dhidi ya magonjwa bado ni silaha muhimu zaidi katika kulinda afya za wananchi.
Wataalamu wa kimataifa pia wameonyesha matumaini kuhusu matumizi ya Akili Unde katika utafiti wa chanjo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Chanjo ya Oxford, Profesa Andy Pollard amesema matokeo ya awali yanaonyesha ishara nzuri katika majaribio ya wanyama na kwamba AI inaweza kusaidia kutabiri kwa haraka namna mfumo wa kinga utakavyoitikia chanjo.
Kwa upande wake, Profesa Marian Knight wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Masuala ya Afya amesema mafanikio hayo yanaweza kuwa mwanzo wa maendeleo makubwa katika utengenezaji wa chanjo zinazotoa kinga pana na ya muda mrefu dhidi ya virusi mbalimbali.
Naye Waziri wa Sayansi wa Uingereza, Lord Vallance amesema mafanikio hayo yanaonyesha jinsi teknolojia ya Akili Unde inavyoweza kuunganishwa na utafiti wa kisayansi ili kuibua matibabu na chanjo mpya zenye manufaa kwa jamii.
Licha ya matumaini hayo, watafiti wameonya kuwa bado kuna hatua nyingi za kisayansi na kisheria zinazopaswa kukamilishwa kabla chanjo hiyo haijaanza kutumika kwa umma.
Hata hivyo, matokeo ya awali yanaashiria mwanzo wa enzi mpya katika matumizi ya Akili Unde katika mapambano dhidi ya magonjwa hatari duniani, yakiwemo Ebola na virusi vingine vinavyoendelea kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu.