Kiungo gwiji na nguli wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes, amemlipua hadharani mchezaji mwenzake wa zamani, Cristiano Ronaldo, akisema kuwa mchezaji mwenye umri wa miaka 41 anapaswa kuanza kwenye nafasi moja tu uwanjani nayo ni ya golikipa.

Kauli hiyo kali imekuja wakati huu ambapo timu ya taifa ya Ureno iko vitani kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026 linalofanyika katika nchi za Marekani, Canada, na Mexico, huku mjadala mkubwa ukitawala kama ni sawa au sio sawa kwa Ronaldo mwenye umri wa miaka 41 kuendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo ya Ulaya.

Scholes anaona kuwa kasi, nguvu, na presha ya soka la kisasa katika ngazi ya Kombe la Dunia ni kubwa mno kwa mchezaji wa kawaida wa uwanjani mwenye umri mkubwa kama huo kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

 Scholes anaamini kuwa nafasi pekee ya mchezaji mwenye umri wa miaka 41 kama Ronaldo ni nafasi ya golikipa pekee.

Scholes katika maoni yake akiwa anachambua hoja hiyo, hakung’ata maneno kuhusu uamuzi wa Kocha wa Ureno, Roberto Martínez, kuendelea kumtegemea CR7 kama nguzo kuu ya mashambulizi.

“Ukiwa na umri wa miaka 41, naamini kuna nafasi moja tu uwanjani ambayo mchezaji wa umri huo anapaswa kuanza kikosini. Nayo ni ya golikipa, kwa mtazamo wangu,” amesisitiza Scholes.

Scholes ametolea mfano wa makipa wakongwe kama Vozinha wa Cape Verde anayeng’ara kwenye Kombe hili la Dunia akiwa na miaka 40, akieleza kuwa makipa hawatumii nguvu nyingi za kukimbia uwanja mzima ikilinganishwa na washambuliaji wanaotakiwa kukabiliana na mabeki vijana, wenye kasi na nguvu zote.

Ronaldo anajibu kwa mabao?

Licha ya ukosoaji mkubwa kutoka kwa wachambuzi wa soka Ulaya, Cristiano Ronaldo bado anaendelea kuthibitisha kuwa yeye ni kiumbe wa kipekee wa kibaolojia.

Ronaldo amekuwa akipambana kulinda nafasi yake mbele ya washambuliaji vijana wenye njaa ya mafanikio kama Gonçalo Ramos.

Mvuto wa kibiashara, kisaikolojia

Uwepo wa Ronaldo uwanjani bado unatoa hofu kubwa kwa mabeki wapinzani na unaleta hamasa ya kipekee jukwaani, jambo ambalo kocha Martínez analitumia kama silaha ya kisaikolojia.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *