Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kuongezeka kwa wapiganaji wa kundi la waasi la RSF, ambao wameuzingira mji wa El Obeid nchini Sudan.

 Wajumbe hao wameonya kuwa mashambulizi ya nchi kavu dhidi ya mji huo yanaweza kuwaweka maelfu ya raia katika hatari kubwa. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, wajumbe hao wameonya kuhusu hatari ya karibu ya kutokea kwa mauaji ya halaiki na kuitaka RSF kusitisha mara moja mashambulizi yake dhidi ya El Obeid.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza hilo pia limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa mapigano katika maeneo mbalimbali ya Sudan, hususan katika majimbo ya Kordofan, ambako ongezeko la mapigano linatishia kuzidisha zaidi hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari inaikabili nchi hiyo. Wajumbe wa Baraza walizitaka pande zote zinazohusika katika mzozo huo kusitisha mara moja mapigano ili kuzuia kuendelea kwa mateso ya raia.

Baraza hilo limeonya kuhusu uwezekano wa kurudiwa kwa maovu yaliyoripotiwa wakati waasi wa RSF walipoteka mji wa Al-Fashir katika eneo la Darfur mwishoni mwa mwaka uliopita. Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, zaidi ya watu 6,000 waliuawa mjini humo katika kipindi cha siku tatu.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza tena dhamira yao ya kuunga mkono mamlaka, uhuru, umoja na ukamilifu wa eneo la Sudan. Pia wamekataa vikali juhudi zozote za kuanzisha mamlaka mbadala ya utawala katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa RSF. Baraza hilo limezitaka nchi zote kutekeleza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa pamoja na kutekeleza maazimio husika ya Baraza la Usalama, ikiwemo Azimio namba 2791 la mwaka 2025, huku juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini Sudan zikiendelea.

Mapigano nchini Sudan yalianza Aprili 2023 kati ya Jeshi la Serikali na waasi wa RSF wanaotaka kunyakua Madaraka. Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa ndie muungaji mkono mkuu wa waasi hao wa RSF wanaotenda jinai nchini humo.

Umoja wa Mataifa umeelezea mzozo huo kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni 11.5 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano, huku takribani nusu ya wakazi wa Sudan wakikabiliwa na njaa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *