Muungano maaskofu wa kanisa Katoliki (CENCO) umepinga mapendekezo ya kuifanyia marekebisho katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Uamuzi huu umetolewa baada ya maaskofu hao kuwa na majadiliano ya siku tatu kuhusiana na suala hilo tata.

Lengo kuu la majadiliano yaliyoongozwa na maaskofu hao lilikuwa ni kufanya maamuzi kuhusu suala hilo la mageuzi ya katiba ya Kongo.

Maaskofu hao walisikiliza maoni kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na wale wa upande wa rais Félix Tshisekedi pamoja na wataalamu na wasomi wa masuala ya katiba kabla ya kufanya uamuzi wao.

Wanasiasa kutoka mrengo wa Rais wa Kongo Félix Tshisekedi  wanaunga mkono mapendekezo ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi.

Upinzani nao unaona kwamba mrengo unaomuunga mkono Rais Tshisekedi unatumia nafasi hiyo ya kufanyia katiba marekebisho kama njia moja ya kumfanya rais Tshisekedi kuendelea kusalia madarakani.

“Hatuoni haja wala dharura au nafasi ya kufanyika kwa mageuzi ya katiba.” ilisema taarifa ya maaskofu hao iliosomwa na katiba wao Mkuu Askofu Donatien Nshole.

Viongozi hao wa kidini wametoa wito kwa Rais wa DRC kuheshimu kiapo chake na kuitetea katiba.

Askofu Donatien Nshole, aidha amesisitiza kwamba kanisa halitojiunga na upinzani lakini litaendelea kuwa na uaminifu kwa mojawapo ya kanuni zake, kuheshimu mpangilio wa kikatiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *