Mbeya. “Free Lissu, Free Lissu, Free Lissu” zikiashiria Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Ni sauti za wananchi na wafuasi wa Chadema zilizotawala katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya wakati wa mkutano wa chama hicho.

Chadema ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake Taifa, John Heche, wameendelea na ziara yao mkoani Mbeya, huku ikitangaza mambo mawili ambayo ni Katiba Mpya na Free Lissu, ambapo kesho ziara hiyo itakuwa Tunduma mkoani Songwe.

Katika mkutano huo uliofanyika leo Juni 23, aliyekuwa Katibu wa Chama cha Ukombozi wa Umma Mkoa wa Mbeya (Chaumma), Patrobas Mgimbila, ametangaza kurejea tena Chadema huku akiomba radhi kwa wafuasi na chama hicho.

Wananchi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika mkutano wa Chama hicho uliofanyika katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya katika mwendelezo wa ziara ya Chama hicho.

“Nilitoka Chadema nikaenda upande mwingine kwa sababu fulani, ila moyo wangu ulinihukumu. Naomba kurejea tena mnipokee,” amesema Mgimbila akishangiliwa na kupokelewa.

Akizungumza katika mkutano huo, akinukuu baadhi ya vifungu vya Katiba, Heche amesema ukubwa wa Tanzania unaunganisha zaidi ya mataifa matatu, Kenya, Uganda na Burundi, ikiwa ni utajiri wa kwanza, lakini nchi hiyo pia ni ya tatu kuwa na madini mengi kila kona.

Amesema rasilimali ilizonazo Tanzania ikiwamo Ziwa Tanganyika, mlima mrefu Afrika wa Kilimanjaro, mbuga, lakini imekuwa nchi yenye umasikini na kukosa huduma muhimu za kijamii kama afya, na kuhoji matabaka ya wenye nacho na wasio nacho huku akibainisha mambo manne.

“Tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na lazima tuondoe viongozi wasio waadilifu na ili kutekeleza hayo lazima tupate Katiba Mpya, hakutakuwapo kukosekana kwa haki.

“Kwa mujibu wa Katiba tuliyonayo, ardhi ni mali ya Rais, kwa maana hiyo anayo mamlaka yote kufanya kila kitu. Maumivu ni makubwa kupitia Katiba hii na ndiyo maana kipaumbele chetu cha kwanza ni Katiba Mpya,” amesema Heche.

Amesema kwa sasa nchi inayotakiwa ni ile ambayo mtu yeyote anaweza kupata haki yake kulingana na uwezo alionao badala ya upendeleo na kwamba Tanzania ina watu wengi na siyo kutegemea familia moja, akitolea mfano wa mfumo wa uteuzi wa viongozi wa Serikali nchini Kenya.

Wananchi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika mkutano wa Chama hicho uliofanyika katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya katika mwendelezo wa ziara ya Chama hicho.

“Tujiulize kwa mshangao, iweje shule za binafsi, hospitali binafsi zinazolipa kodi, zinanunua ardhi zifanye vizuri kuliko Serikali ambayo hailipi kitu zifanye vibaya, lazima tubadilike,” amesema Heche.

Amesema Serikali ya Tanzania inashindwa kuendelea kutokana na kuchaguana, kutokana na baadhi ya watu kujipendekeza kwa viongozi, na kwamba kwa rasilimali za Tanzania zilipaswa kuwafanya Watanzania kuwa matajiri.

“Mfano tunazo bandari na zipo nchi ambazo hazina mlango wa bahari ambazo zikitumia vyema bandari zetu kuchukua mizigo kwa kujenga gati.

Amesema kwa sasa Chadema wako “serious” (makini) na ukombozi wa nchi, akionesha kusikitishwa na baadhi ya wabunge wanaodai kuwatoza bodaboda fedha kwa ajili ya kujenga barabara.

Dini na siasa

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mzee, amekemea baadhi ya watu kuingiza masuala ya dini na siasa akieleza kuwa mambo hayo yakiingiliana kutakuwa na mpasuko mkubwa.

Ametuma salamu kwa Jeshi la Polisi akieleza kuwa hawajasikia kauli yao ya kulaani maneno ya baadhi ya watu wanaochochea na kuwaomba Watanzania kuwapuuza.

“Tunaomba hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya mtu huyo, hatutasita kulaani kauli za hivyo za kuweza kutugawa, tumkatae na kulaani kugawanyika kwa misingi ya dini, vinginevyo Taifa litagawanyika.

Wananchi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa katika mkutano wa Chama hicho uliofanyika katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya katika mwendelezo wa ziara ya Chama hicho.

“Sisi Zanzibar tumekuwa tunapigania Muungano wa serikali tatu, tunawabebesha mzigo mkubwa, Zanzibar ikikopa Bara ndiyo mnalipa, wao wanasema bajeti yao ni ndogo, hata pesa zenu ndizo zinawapigia kura CCM,” amesema Mzee.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (Bavicha), Michael Kitiga, ametaja mambo matatu yaliyowaleta mkoani Mbeya ambayo ni uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliodai kupoteza sifa na badala yake wanalindwa na vyombo maalumu.

“Jambo la kwanza hatuna ugomvi na Polisi, jambo la pili tunataka Katiba Mpya, tatu tunaungana na wananchi wengine wote wa Tanzania kwa ujumla kudai haki yetu na kuachiwa huru Lisu,” amesema Kitiga.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Taifa, Elizabeth Mwakimomo, amesema Oktoba 29, Mkoa wa Mbeya haukushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu na kwamba Chadema itaendelea kudai na kupigania haki.

“Tuna changamoto ya vumbi ya miaka mitatu hapa Mbeya mjini, tulikuwa na barabara moja ambayo bora ingebaki vilevile kuliko hiki kilichofanyika,” amesema Elizabeth.

Katibu wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amesema Mbeya wako imara kulinda chama hicho na kwamba wafuasi na wananchi kwa ujumla wamekuwa wahanga.

Amewataka Jeshi la Polisi kufanya kazi yao kwa weledi badala ya kuelekezwa na baadhi ya viongozi wa siasa akieleza kuwa Chadema itakaposhika dola itawabadilishia maisha.

“Mbeya tuko imara kulinda chama chetu, tumekuwa wahanga ambapo baadhi ya makada wetu wamekamatwa hadi sasa kwa kutoa maoni yao, tuombe Polisi wafanye kazi yao,” amesema Mbeyale.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *