Zaidi ya wakimbizi milioni 1.3 wa Sudan wanaishi Cairo, mji mkuu wa Misri kwa hofu na wasiwasi mkubwa, na licha ya mabilioni ya dola ya misaada yanayotumwa kwa nchi hiyo, wengi wao wanaendelea kufanya jitihada za kuondoka Misri kutokana na hofu ya kukamatwa na kufungwa.

Ripoti ya Shirika la Habari la Iran (IRNA), imenukuu kituo cha televisheni cha Ujerumani cha Tagesschau kwamba, zaidi ya wakimbizi milioni 1.3 wa Sudan wanaishi Cairo pekee na kwamba serikali haiwapi hifadhi katika kambi maalumu; badala yake, wanakodisha vyumba katika mji mkuu na kupata riziki kutokana na kazi za kawaida.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wakimbizi hao wanazidi kushambuliwa na serikali ya Misri, kukamatwa kiholela na kufukuzwa nchini huko, huku Misri ikidai inafanya kila iwezalo kuhakikisha ustawi wa “ndugu zake wa Sudan.”

Hata hivyo wengi kati ya wakimbizi hao waSudan wanasema wanasumbuliwa sana na vyombo vya usalama vya Misri na kwamba wanashindwa kufanya kazi ya kujikimu kimaisha kutokana na kuandamwa na askari usalama wa Misri.

Maryam, mwanamke kijana wa Sudan ambaye amekuwa akiishi Cairo, mji mkuu wa Misri, kwa miezi kadhaa baada ya kukimbia vita vya ndani nchini Sudan anasimulia kwamba: “Hali nchini Sudan ilikuwa mbaya na ngumu sana. Ndiyo maana tumekimbia, tukiwa na matarajio ya kuendelea na masomo na kufanya kazi nchini Misri.” Maryam anasema: Hata hivyo Ulimwengu mpya wa wakimbizi wa Sudan sio kile walichokiota na kukitarajia.

Anasema: “Dada zangu hawawezi kwenda shule. Wanakaa nyumbani siku nzima. Watoto hawaruhusiwi kusoma katika shule ya Misri kwa sababu hawana hadhi rasmi ya ukaazi na hakuna shule za wakimbizi katika eneo latu.

Mkimbizi mwingine wa Sudan aliyejutambulisha kwa jina la Ahmed anasema kwamba wakimbizi wanaishi kwa woga na hakuna anayetaka kuondoka majumbani mwao tena kwa sababu wanakamatwa, wanatupwa gerezani na kufukuzwa mara moja, bila kuruhusiwa kuonana na watoto wao tena.

Haya yanaripotiwa huku wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakieleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu taarifa za kuongezeka wapiganaji wa kundi la waasi la RSF, ambao wameuzingira mji wa El Obeid nchini Sudan.

Baraza hilo pia limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea mapigano katika maeneo mbalimbali ya Sudan, hususan katika majimbo ya Kordofan, ambako ongezeko la mapigano linatishia kuzidisha hali mbaya. Wajumbe wa Baraza la Usalama wamezitaka pande zote zinazohusika katika mzozo huo kusitisha mara moja mapigano ili kuzuia mateso ya raia.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *