Sudan Kusini imetangaza kuwa itafanya uchaguzi wake mkuu wa kwanza tarehe 22 Desemba mwaka huu, baada ya miaka mingi ya kuahirishwa mara kwa mara tangu nchi hiyo ilipojitangazia uhuru, zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imethibitisha tarehe hiyo, ikisema kuwa maandalizi yanaendelea kote nchini humo, licha ya kuendelea mzozo wa silaha na changamoto mbalimbali za kilojistiki.

Sudan Kusini ilitangaza uhuru wake mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan. Imekuwa ikiongozwa chini ya mpango wa kugawana madaraka tangu mwaka 2018, kama sehemu ya mkataba wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano vilivyochochewa na mgogoro kati ya Rais Salva Kiir Mayardit na kiongozi wa upinzani Riek Machar. Machar aliwahi kuhudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kiir hadi aliposimamishwa kazi baada ya kushtakiwa kwa uhaini. Kwa sasa, yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

Nchi hiyo isiyo na mipaka ya bahari imekuwa na hali tete tangu kumalizika vita vya ndani, huku mivutano ya kisiasa ikiongezeka katika miezi ya hivi karibuni kufuatia kufutwa kazi na kukamatwa maafisa wanaodaiwa kuwa waaminifu kwa Machar.

Serikali ya mpito imeakhirisha uchaguzi kwa uchache mara tano, ambapo uchaguzi wa awali ulipaswa kufanyika mwaka 2015 na baadaye kusukumwa hadi 2018, 2021, 2023, kisha 2024.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Sudan Kusini, Abednego Akok Kacuol, amesema tume hiyo inahitaji dola milioni 250 kuendesha uchaguzi wa mwaka 2026, lakini hadi sasa imepokea sehemu ndogo tu ya fedha zinazohitajika.

Serikali imesisitiza kuwa uchaguzi utaendelea kama ilivyopangwa bila kuahirishwa zaidi, licha ya kuongezeka wasiwasi kuhusu ukosefu wa utulivu wa kisiasa, mapigano ya mara kwa mara na kuhama makazi kwa raia kote nchini.

Chama cha upinzani cha -Upinzani (SPLM-IO cha Machar, kimeonya kuwa changamoto za kiusalama ambazo hazijatatuliwa na mivutano na utawala wa Kiir inafanya uchaguzi kuwa jambo hatari.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, kaimu mwenyekiti wa SPLM-IO, Nathaniel Pierino, alisema: “Yeyote atakayekuja kusajili wapiga kura na kufanya kampeni katika maeneo yanayodhibitiwa” na kundi hilo atatambuliwa kama “mfungwa wa kivita, au atauawa.”

Pierino alionya: “Kufanya uchaguzi ili kuvunja [mkataba wa amani wa 2018] kwa Sudan Kusini ni… siasa tupu, si utawala bora; na jambo hilo litaitumbukiza nchi katika machafuko zaidi.”

Rais Kiir anatarajiwa kugombea katika uchaguzi wa urais wa mwezi Desemba. Haijulikani kama Machar ataruhusiwa kugombea kutokana na mashtaka ya jinai yanayomkabili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *