
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema kuwa Marekani ina wajibu wa kuondoa vikwazo vyote vya kiuchumi ilivyoiwekea Iran kinyume cha sheria, kulingana na mkataba wa maelewano uliotiwa saini kati ya Iran na Marekani.
Katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari uliofanyika siku ya Jumanne, afisa huyo alisema: “Wajibu wa Marekani uko wazi: Kuondoa vikwazo vya msingi, vya upili, vile vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na vile vinavyohusiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).”
Kauli hizo zilihusu Ibara ya Saba ya mkataba wa maelewano uliopatanishwa na Pakistan ambao ulitiwa saini hivi karibuni na marais wa Iran na Mareknai. Kama sehemu ya kipengele hicho, vikwazo vyote dhidi ya Iran lazima viondolewe.
Baghaei ameashiria pia kuhusu leseni iliyotolewa awali na Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) ya Wizara ya Hazina ya Marekani, inayotoa nafuu ya vikwazo kwa sekta ya mafuta, petrokemikali, na bidhaa za Iran kwa kipindi cha siku 60. Amesema, “Vikwazo vingine vitajadiliwa ndani ya kipindi hicho cha siku 60.”
Msemaji huyo alizungumzia msisitizo wa Iran, kama sehemu ya mapatano hayo, juu ya kusitishwa kwa uchokozi katika pande zote, ikiwemo Lebanon. Ameelezea uamuzi uliofanywa wakati wa duru ya kwanza ya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa mkataba huo nchini Uswisi, kwa ajili ya kuanzishwa kwa “kitengo cha kuzuia migogoro” (deconfliction cell) ili kusaidia kuimarisha usitishaji wa mapigano nchini Lebanon.
Msemaji huyo, wakati huo huo, amejibu madai kuhusu majadiliano ya mpango wa makombora ya ulinzi ya Iran nchini Uswisi. Amesisitiza kuwa: “Suala la makombora ya Iran na uwezo wake wa ulinzi halijawahi kuwa sehemu ya mazungumzo na halitakuwa kamwe.”
Kuhusu suala la nyuklia, Baghaei amesema mada hiyo haikuibuka wakati wa mazungumzo ya Uswisi na imepangwa “kuchunguzwa ndani ya kipindi cha siku 60.” Aidha amesisitiza kuwa “hatuna mpango wowote wa kuruhusu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kukagua vituo vya nyuklia vilivyoharibiwa wakati wa uchokozi wa Marekani na Israel.”
Kuhusu hali ya vikosi vya Marekani katika kanda, Baghaei amebainisha kuwa, kama sehemu ya mkataba huo, vikosi vya Marekani vinatakiwa kuondoka katika maeneo yanayozunguka Iran ndani ya siku 30 baada ya makubaliano ya mwisho. Kuhusu dhamana na utekelezaji, msemaji huyo alisema Iran imetumia zana zote ilizo nazo kuhakikisha pande zote zinatekeelza ahadi zao.