Dar es Saaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mikopo inayopatikana kutoka kwa wahisani na taasisi mbalimbali za maendeleo ndiyo iliyobadilisha taswira ya nchi, baada ya kufanya mageuzi ya miundombinu nchini.
Amesema miradi inayotekelezwa kwa fedha hizo za mikopo, ikiwemo ya miundombinu ya barabara, imeleta matokeo katika maisha ya wananchi wa sasa na itaendelea kunufaisha vizazi vijavyo.
Amesema ni fedha hizo za mikopo zilizobadili hata miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mradi wa DMDP.
Mwonekano wa Barabara ya mzunguko ya Dodoma.
Februari 20, 2024 Serikali ilisaini mkopo wa takriban Sh1 trilioni na Benki ya Dunia (WB) kutekeleza mradi huo ambao umeboresha barabara zenye urefu wa kilomita 250 katika manispaa zote tano za Kinondoni, Ilala, Kigamboni, Ubungo na Temeke, ikilinganishwa na kilomita 207 zilizotekelezwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo kwa wilaya tatu pekee.
Ulega ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma, wiki hii wakati wa mjadala wa masuala ya maendeleo ya taifa.
Amesema fedha za mikopo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo isingeweza kutekelezwa kwa urahisi kwa kutumia mapato ya ndani pekee.
Katika sekta ya ujenzi, amesema Tanzania imeendelea kushuhudia miradi mbalimbali ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege ikikamilika, huku mingine ikiwa katika hatua tofauti za utekelezaji, jambo ambalo limeongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Ulega, manufaa ya miradi hiyo yanaonekana wazi katika maeneo mengi ya nchi, ambapo wananchi wamepata urahisi wa usafiri na usafirishaji, huduma za kijamii zimefikiwa kwa urahisi zaidi na shughuli za kiuchumi zimeongezeka kutokana na kuimarika kwa miundombinu.
“Nchi inajengwa kama mnavyoona. Madaraja yanajengwa, barabara zinajengwa na mikoa inafunguliwa na kuunganishwa na mingine. Hatuchukui mikopo kwa sababu ya watu wanaoishi sasa pekee, bali pia kwa ajili ya vizazi vijavyo ili nao wakija waseme wazazi wao walitendea haki taifa lao na fedha walizokopa,” amesema.
Waziri huyo, amesisitiza kuwa mikopo ya maendeleo imekuwa nyenzo muhimu ya kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye tija kwa taifa na kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila fedha zinazokopwa zinaleta matokeo yanayopimika kwa wananchi.
Moja ya kituo cha BRT Awamu ya Tatu inayoanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la Mboto .
Akifafanua zaidi, Ulega alitolea mfano Programu ya Ujenzi wa Dharura wa Madaraja (CERC) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambapo hadi sasa mikoa 22 imenufaika kupitia miradi 81 ya madaraja na vivuko.
Amesema kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo, mawasiliano yalikuwa yakikatika baadhi ya maeneo wakati wa mvua kutokana na kuharibika kwa miundombinu. Hata hivyo, ujenzi wa madaraja hayo umeondoa changamoto hiyo na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao bila usumbufu.
Ulega pia ametaja miradi iliyowezeshwa na mikopo ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, Daraja la Pangani, Barabara ya Mnivata–Mnitesa mkoani Mtwara pamoja na Barabara ya Kasulu–Manyovu mkoani Kigoma.
Kwa upande wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), amesema taasisi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya usafiri kupitia ufadhili wa ujenzi wa barabara za mzunguko za Jiji la Dodoma, upanuzi wa barabara za Moshi Mjini kuwa njia nne na maboresho ya Barabara ya Arusha–Moshi–Himo.
“Hakuna hata senti moja inayoingia Tanzania kama mkopo ambayo hainufaishi maisha ya Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo. Huo ndiyo ukweli,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Ujenzi, taasisi nyingine za maendeleo zimeendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ambalo limechangia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam, hususan katika njia za Ubungo–Bandari na Tabata–Kigogo.
Aidha, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) imechangia ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Tabora, Kigoma, Shinyanga na Sumbawanga, hatua ambayo imeongeza uwezo wa viwanja hivyo kuhudumia wasafiri na kuchochea shughuli za biashara na utalii katika maeneo husika.
Miundombinu ya Barabara ya Ubungo-Kimara.
Ulega, amesema matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana wazi katika mikoa mingi iliyokuwa nyuma kimaendeleo kutokana na changamoto za miundombinu.
Ametaja Kigoma kuwa mfano wa maeneo ambayo kwa miaka mingi lilikuwa na changamoto za kuunganishwa kwa urahisi na sehemu nyingine za nchi.
“Miaka michache iliyopita, Kigoma ilikuwa imeunganishwa kwa kiwango kidogo sana na mikoa mingine ya Tanzania. Leo hii imefunguka kwa kiasi kikubwa na sehemu ya mafanikio hayo imetokana na uwekezaji uliofanywa kupitia mikopo ya maendeleo,” amesema.
Pia, amezungumzia ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam unaofadhiliwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia, akisema mradi huo utakapokamilika utatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya mafuriko yaliyokuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo kila msimu wa mvua.
Kwa ujumla, Serikali inaamini kuwa matumizi ya mikopo ya maendeleo katika miradi ya kimkakati yamekuwa msingi muhimu wa kuharakisha ukuaji wa uchumi, kuboresha huduma kwa wananchi na kujenga miundombinu imara itakayonufaisha Tanzania kwa miongo mingi ijayo.