Mwanza.  Wafanyabiashara jijini Mwanza wametakiwa kuacha tabia ya kuwatumia watoto kuuza mifuko na kubeba mizigo sokoni, kwa kuwa vitendo hivyo vinachangia ukatili dhidi yao, kuwanyima haki ya kupata elimu na kuwakosesha malezi bora.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Juni 25, 2026 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha malezi bora, kupinga mmomonyoko wa maadili na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoani Mwanza, uliofanyika katika Soko la Mirongo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mwenyekiti mwenza wa kamati ya mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (Mtakuwwa) Mkoa wa Mwanza, Yasini Ally amesema moja ya changamoto kubwa iliyobainika ni ongezeko la watoto wanaozagaa masokoni wakijihusisha na biashara ndogondogo badala ya kuwa shuleni.

Mfanyabiashara wa tikiti maji soko la Mirongo, Issa Maduli akizungumzia athari za ukatili kwa watoto katika familia.

“Leo moja ya changamoto iliyoibuliwa na wafanyabiashara wa soko hili ni wimbi kubwa la watoto wadogo wanaojihusisha na biashara ya kuuza mifuko na kubeba mizigo badala ya kuwa shule,” amesema Ally.

Amesema tatizo hilo halipaswi kuonekana kuwa la kawaida kwa kuwa ni sehemu ya ukatili dhidi ya watoto unaowanyima fursa ya kupata elimu na malezi stahiki.

“Tunapozungumzia ukatili dhidi ya watoto, tunamaanisha pia mifumo inayowafanya washindwe kwenda shule na badala yake kujikuta wakifanya biashara masokoni. Hii ni changamoto inayohitaji hatua za pamoja,” amesema.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha jamii kubadili mtazamo na kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya malezi bora na elimu, huku akisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mwanajamii.

Mkaguzi wa Kata ya Mirongo, Fatuma Mpingo, amesema wafanyabiashara wana nafasi kubwa ya kusaidia kutokomeza hali hiyo kwa kubadili namna wanavyouza bidhaa zao.

“Wafanyabiashara waweke mifuko kwenye meza zao badala ya kuwatumia watoto. Hii ni mojawapo ya aina ya ukatili tunaoupinga,” amesema.

Askofu Robert Bundala, Mjumbe wa MTAKUWWA Mkoa wa Mwanza, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha malezi bora, kupinga mmomonyoko wa maadili na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto mkoa wa Mwanza.

Diwani wa Kata ya Mirongo, Nurdini Mbaji, amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwatumia watoto kwa manufaa yao bila kuzingatia haki zao za msingi.

“Wafanyabiashara wanawatumia watoto lakini wanawanyima haki zao. Lazima tuwaondoe watoto hawa hapa sokoni,” amesema.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wameeleza kuwa hali hiyo inachangiwa na changamoto za kiuchumi pamoja na ukosefu wa muda wa kutosha wa kuwalea watoto wao, jambo linalowafanya baadhi yao kuja nao maeneo ya biashara.

Mfanyabiashara, Alex Funya amesema suluhisho la tatizo hilo lipo mikononi mwa wafanyabiashara wenyewe kwa kuhakikisha watoto hawahusishwi katika shughuli za biashara.

“Kila mfanyabiashara awe na mifuko yake na kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kwenda shule,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mwanza, Thabisa Masota, ameonya kuwa watoto wanaokaa masokoni hukutana na mazingira yasiyofaa kwa ukuaji na malezi yao.

“Kuna lugha na mazingira yasiyofaa kwa mtoto. Tunapaswa kuhakikisha watoto wanakuwa katika maeneo salama ya kujifunzia na kulelewa,” amesema.

Akizungumzia changamoto za malezi, mfanyabiashara wa matikiti maji, Issa Maduli amesema shughuli za kutafuta riziki zimekuwa zikisababisha baadhi ya wazazi kushindwa kutumia muda wa kutosha na watoto wao.

“Unatoka alfajiri kwenda kutafuta riziki na unarudi usiku mtoto tayari amelala. Hii ni changamoto inayowakabili wazazi wengi,” amesema.

Naye mfanyabiashara wa kuku, Anastazia Mwita amesema mazingira ya biashara huwafanya wazazi kuwa mbali na watoto wao kwa muda mrefu, hali inayoweza kuathiri malezi yao.

“Wakati mwingine mtoto anabaki na mfanyakazi wa nyumbani kwa muda mrefu na kukosa uangalizi wa karibu wa mzazi,” amesema.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, uongozi wa Soko la Mirongo umeanza kuhamasisha wafanyabiashara kuwa na mifuko yao wenyewe ili kuondoa utegemezi wa watoto katika biashara hiyo.

Pia wazazi wametakiwa kuwapeleka watoto wadogo katika kituo cha malezi kilichojengwa na Shirika la Kivulini wakati wa saa za kazi badala ya kuwaacha wakizurura sokoni.

Mtendaji wa Kata ya Mirongo, Simoni Fulko amesema kituo hicho kitasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaozurura na kufanya biashara sokoni.

Amesema zaidi ya watoto 80 wamebainika wakizurura katika Soko la Mirongo wakijihusisha na biashara ya mifuko na ubebaji wa mizigo.

“Badala ya kuzunguka sokoni, watakuwa katika kituo hicho wakipata malezi na maandalizi ya elimu. Watakapofikia umri wa kuanza shule ya msingi, wazazi wao watawaandikisha rasmi,” amesema.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Mwanza, Faraja Mkinga amewataka wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *