
Watu wengi wanapopata fedha, lengo lao kubwa huwa kununua vitu vitakavyowapa raha ya muda mfupi. Wengine hununua magari ya gharama kubwa, simu za kisasa au kufanya matumizi makubwa ya anasa. Ingawa hakuna ubaya wa kufurahia matunda ya kazi yako, ni muhimu kuelewa kanuni moja muhimu sana ya utajiri, mali yako inapaswa kuzaa mali nyingine.
Kwa lugha rahisi, mali nzuri ni ile inayokuletea mapato au inayokuwezesha kupata mali nyingine zaidi. Watu wengi matajiri duniani hawakufikia mafanikio kwa sababu ya kufanya kazi kwa bidii pekee. Walijenga mfumo ambao mali zao ziliendelea kuzalisha mali nyingine mwaka baada ya mwaka.
Tuchukue mfano wa mkulima anayenunua ng’ombe wa maziwa. Ng’ombe huyo si mali tu kwa sababu ana thamani ya kuuzwa. Ni mali kwa sababu anazalisha maziwa kila siku. Fedha zinazopatikana kutokana na maziwa zinaweza kutumika kununua ng’ombe mwingine. Baada ya muda, ng’ombe mmoja anakuwa wawili, wawili wanakuwa wanne, na mali inaendelea kukua. Huu ndio mfano wa mali inayozalisha mali nyingine.
Mfano mwingine ni mtu anayenunua nyumba ya kupangisha. Kila mwezi nyumba hiyo huleta kodi. Badala ya kutumia kodi yote kwa matumizi ya kawaida, sehemu ya fedha hizo inaweza kuwekwa pembeni ili kununua kiwanja kingine au kujenga nyumba nyingine. Hivyo nyumba ya kwanza inasaidia kuzalisha nyumba ya pili. Mali moja inakuwa chanzo cha mali nyingine.
Kanuni hii inaweza kutumika hata katika uwekezaji wa hisa. Mtu anaponunua hisa za kampuni zinazolipa gawio, anaweza kutumia gawio hilo kununua hisa zaidi. Kadiri muda unavyopita, hisa zinaongezeka na mapato yameongezeka. Hii ndiyo nguvu ya kuifanya mali moja izae mali nyingine.
Watu wengi hufanya kosa la kutumia mapato yote yanayotokana na mali zao kwa matumizi ya kila siku. Matokeo yake, mali inabaki katika kiwango kilekile kwa miaka mingi. Lakini mtu mwenye mtazamo wa kujenga utajiri hutumia sehemu ya mapato hayo kuongeza mali mpya. Hivyo ukuaji wa utajiri wake huwa wa haraka zaidi.
Kanuni hii ni muhimu hata wakati wa kukopa. Watu wengi hukopa kwa ajili ya matumizi ya kawaida au anasa. Wengine hukopa ili kufanya sherehe, kununua vitu vya kifahari au kugharamia matumizi ambayo hayazalishi mapato yoyote. Matokeo yake, mkopo unakuwa mzigo unaohitaji kulipwa kutoka kwenye kipato cha kawaida. Lakini kama mtu atalazimika kukopa, ni busara kukopa kwa ajili ya mali inayoweza kuzalisha mapato. Kwa mfano, mkopo wa kununua mashine ya uzalishaji, kujenga nyumba ya kupangisha, kununua trekta la biashara au kuanzisha mradi wenye uwezo wa kuleta mapato unaweza kuwa na maana zaidi.
Hata hivyo, ni muhimu kuwa makini. Siyo kila kitu kinachoitwa uwekezaji ni mali nzuri. Mali nzuri ni ile inayozalisha mapato au kuongeza thamani kwa muda. Kabla ya kukopa au kuwekeza, jiulize swali moja muhimu: “Je, mali hii itaniletea mapato au itanigharimu fedha zaidi?” Jibu la swali hilo linaweza kuamua mafanikio au matatizo yako ya kifedha.
Watu wengi wenye mafanikio ya kifedha hufikiri tofauti. Wanapotazama fedha, hawaoni tu matumizi ya leo. Wanaona fursa ya kujenga mali itakayozalisha mali nyingine.
Kwa hiyo, kila unapopata fedha, jiulize namna ya kuifanya izalishe mali. Kila unapowekeza, fikiria jinsi uwekezaji huo utakavyokusaidia kujenga uwekezaji mwingine. Siri ya utajiri si kuwa na mali moja kubwa, bali ni kuwa na mali zinazozalisha mali nyingine tena na tena kwa miaka mingi.