Serikali imeombwa kuangalia upya utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wanawake wajane ambao hawana uwezo wa kuanzisha au kuendesha shughuli za biashara zitakazowawezesha kurejesha mikopo hiyo.

Ombi hilo limetolewa wakati wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani lililofanyika katika Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Tawala kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Castori Muhangi, alisema kuwa baadhi ya wajane hukabiliwa na changamoto za kiuchumi zinazowafanya washindwe kunufaika ipasavyo na mikopo inayotolewa kwa makundi maalum.

Alisema kuwa kwa kundi la wajane wasio na uwezo wa kufanya biashara au kurejesha mikopo, Serikali inaweza kuzingatia njia mbadala za kuwawezesha kiuchumi, ikiwemo kuwapatia ruzuku au fedha za kujikimu ili kuwasaidia kukabiliana na mahitaji yao ya msingi.

Muhangi alibainisha kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kuboresha ustawi wa wajane na kupunguza mzigo wa maisha wanaokabiliana nao baada ya kupoteza wenza wao, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya kijamii inayozingatia mazingira halisi ya makundi hayo.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *