Wataalamu wa biashara ya mafuta na bidhaa zake duniani wameonya kuwa nchi nyingi zinazoagiza mafuta kupitia masoko ya kimataifa, hususan zile zinazotegemea kwa kiwango kikubwa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, zinaweza kuchukua kati ya wiki nane hadi kumi kuanza kushuhudia mabadiliko makubwa ya bei za rejareja za mafuta licha ya bei ya mafuta ghafi kuanza kushuka katika soko la dunia.

Tahadhari hiyo inakuja wakati bei ya mafuta ghafi aina ya Brent imeshuka hadi Dola za Marekani 73.49 kwa pipa, kiwango cha chini zaidi tangu kabla ya kuanza kwa vita, baada ya kupanda hadi zaidi ya Dola 100 kwa pipa wakati wa kilele cha taharuki iliyohusisha Iran, Marekani na Israel.

Wachambuzi wanaeleza kuwa kushuka huko kumechangiwa na kupungua kwa hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta, kuendelea kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani pamoja na kurejea kwa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz.

Kwa mujibu wa Reuters, soko la mafuta limeanza kuondoa kile kinachoitwa geopolitical risk premium—gharama ya ziada iliyotokana na hofu ya vita na kukatika kwa usambazaji wa mafuta.

Mlango wa Hormuz unapitia takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani, hivyo kurejea kwa meli za mafuta katika njia hiyo kumeongeza matumaini ya kuimarika kwa upatikanaji wa mafuta na kushusha bei katika masoko ya kimataifa.

Hata hivyo, Reuters inanukuu wataalamu wakieleza kuwa baadhi ya kampuni za usafirishaji na bima bado zinaendelea kuwa waangalifu kutokana na masuala ya usalama, jambo linalomaanisha kuwa kurejea kwa biashara katika hali ya kawaida bado kunahitaji muda.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pia limesema kushuka kwa bei za mafuta na bidhaa nyingine za nishati tayari kumeanza kufuatia kupungua kwa mvutano na maendeleo ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani, lakini limesisitiza kuwa mtiririko wa biashara na bei hauwezi kurejea katika hali ya kawaida kwa muda mfupi. Kwa mujibu wa wataalamu wa sekta ya mafuta, bei za rejareja huchelewa kushuka kwa sababu mafuta hupitia mnyororo mrefu wa biashara unaojumuisha ununuzi wa mafuta ghafi, usafirishaji kwa meli, usafishaji katika viwanda, uhifadhi, usambazaji na hatimaye kuuzwa katika vituo vya mafuta.

Ndiyo maana katika nchi nyingi manufaa ya kushuka kwa bei ya mafuta ghafi huanza kuonekana kwa watumiaji ndani ya wiki nane hadi kumi, kutegemea mfumo wa biashara na upangaji wa bei wa kila nchi.

Akizungumza na Reuters, mchambuzi wa masoko ya nishati wa kampuni ya Rystad Energy, Janiv Shah, alisema kurejea kwa usafirishaji wa mafuta kutoka Ghuba ya Uajemi ndiko kunakoongoza kushuka kwa bei za mafuta katika kipindi hiki.

“Msongamano wa meli katika Ghuba unaendelea kuondolewa, jambo ambalo limeongeza kiasi cha mafuta kinachoingia sokoni.

Pia tunaona miundombinu ya uzalishaji na vituo vya kusafirisha mafuta vikianza kurejea katika shughuli zake za kawaida,” alisema Shah.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *