Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na mkandarasi; Shirika la Uzalishaji Mali JKT (SUMA JKT) leo, tarehe 25 Juni, 2026 kwa mara ya kwanza wamewasha umeme katika kitongoji cha Lumbila katika Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambapo eneo hilo lilikuwa halijapa umeme tangu Tanzania ipate uhuru wake 9 Desemba, mwaka 1961.
Akiongoza hafla hiyo ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Bodi inayoisimamia REA; Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu alisema utekelezaji wa mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote bila kujali umbali na changamoto za kijiografia.
Eneo hili lilikuwa halijawahi kupata umeme kwa zaidi ya miaka 60 tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961. Hafla hiyo ya kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kitongoji cha Lumbila imefanyika katika Kanisa Katoliki la Kitongoji cha Lumbila, hatua iliyopokelewa kwa furaha kubwa na Wananchi wa eneo hilo.
Awali kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mheshimiwa Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, Mhandisi, Thomas Mmbaga amaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Umeme Vijijini alisema, Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji sita vya mwambao wa Ziwa Nyasa umetumia gharama ya Shilingi bilioni 3.124 na kuongeza kuwa hadi sasa mradi umefikia asilimia 67, ambapo vitongoji 3 kati ya 6 vya mwambao wa Ziwa Nyasa vimeshawashiwa umeme.
Mhandisi Mmbaga ameongeza kuwa Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 36.6 za njia za msongo wa kati na kilomita 15.1 za msongo mdogo.
“Mradi unatarajiwa kuwafikia wateja 151 wa njia moja (single-phase) na wateja 9 wa njia tatu (three-phase). Tayari kaya zaidi ya 23 zimeomba kuunganishiwa”. Amekaririwa, Mhandisi, Mmbaga.
(Feed generated with FetchRSS)