Unguja. Wakati programu ya kuimarisha afya ya uzazi na uzazi wa mpango ikihitimishwa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetaja mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka tisa ikiwa ni pamoja na Wananchi 75,802 kufikiwa na huduma hizo.

Vile vile, wateja 13,834 wamepata huduma ya afya ya uzazi baada ya mimba kuharibika, huduma ambazo zimechangia kupunguza madhara na vifo vinavyoweza kuepukika vinavyotokana na changamoto za ujauzito na utoaji mimba usio salama.

Hayo yamebainishwa Juni 26, 2026 na Kaimu waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya wakati akifunga rasmi mradi huo ulioanza mwaka 2017 kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na wadau wengine.

“Hatua ilichangia kuongezeka upatikanaji wa huduma muhimu za afya ya uzazi kwa wanawake, vijana, na familia kwa ujumla,” amesema Dk Saada

Amesema katika kuimarisha mifumo ya kinga dhidi ya ukatili wa kijinsia, watu 20,336 wamefanyiwa uchunguzi wa ukatili wa kijinsia ambapo 5,421 wamepata ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto wametambuliwa na wahusika kupatiwa huduma stahiki za kitabibu, ushauri nasaha, na rufaa pamoja na miongozo.

Dk Saada amesema programu hii pia imeweka mkazo katika kuyafikia makundi maalum ambapo vijana 949 walifikia huduma za uzazi wa mpango kupitia huduma rafiki kwa vijana, huku watu wenye ulemavu 273 wakipatiwa huduma hizo kwa kuzingatia misingi ya usawa, ujumuishi na haki za binadamu.

Kwa upande mwingine, wahudumu wa afya 554 wamepatiwa mafunzo na kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali ya afya ya uzazi, uzazi wa mpango, huduma baada ya kuharibika mimba, pamoja na mwitikio dhidi ya ukatili wa kijinsia.

“Kwa hiyo, uwekezaji huu katika rasilimali watu umeacha msingi imara wa kuendelea kutoa huduma bora hata baada ya kukamilika kwa programu hii. Takwimu hizi ni ushahidi wa wazi wa mchango wa programu hii katika kuimarisha upatikanaji wa huduma na kujenga uwezo wa mifumo ya afya,” amesema.

Naye Mkurugenzi Tiba Wizara ya Afya, Dk Msafiri Marijani, amesema mradi huu umeleta mabadiliko makubwa katika mapambano dhidi ya kuzuia vifo vya mama na mtoto.

“Kama tunavyojua, uzazi wa mpango ni moja ya nguzo muhimu katika kupambana na vifo vya mama na mtoto,” amesema Dk Marijani.

Amesema lengo la kuimarisha uzazi wa mpango siyo kuzuia wananchi kwamba wasizae; “hatuzuii ile haki ya msingi ya wananchi kupata watoto idadi wanayotaka, lengo kuu ni kupata watoto kwa kiasi fulani kwa uwezo ambao unawekwa, namna ambavyo unaweza ukawahudumia, ukawapa mahitaji yao muhimu, lakini vile vile wakae na afya bora.”

Amesema wakipatikana watu wenye elimu na wana afya bora, watasaidia kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinajitokeza kwenye nchi.

Mkurugenzi wa Maendeleo, Serikali ya Uingereza, Anna Wilson amesema bado kuna kazi nyingi ya kufanywa kwani asilimia ya wanawake wanaotumia mbinu za uzazi wa mpango haijabadilika sana tangu 2017, na mahitaji ambayo hayajatimizwa kwa upande wa baba ni takriban asilimia 25, na kundi hili liko ndani ya uwezo wetu kulifikia.

Hata hivyo, amesema itahitaji motisha ya kutosha, rasilimali, na ushirikiano kufikia huko.

“Kwa hivyo leo, tunaposherehekea mafanikio yote, nilitaka pia kueleza mtazamo wa Serikali ya Uingereza kwa ajili ya mbele. Na katika kufanya hivyo, hatuwezi kuyapuuza mabadiliko katika mazingira ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kifedha na kupungua kwa misaada ya maendeleo ya nchi za nje duniani kote, ambayo inamaanisha mabadiliko katika namna ya kufanya kazi,” amesema

Naye Mkuu wa Mawasiliano UNFPA, Dk Warren Bright amesema lengo kubwa la mradi huo ilikuwa ni katika kutekeleza vipaumbele vya UNFPA kuelekea mwaka 2030 malengo ya dunia, hasa katika lengo namba tatu la afya na ustawi.

Amesema wameangazia pia katika kipaumbele cha kuhakikisha yale mahitaji muhimu na ya hiari ya uzazi wa mpango yanamfikia kila muhitaji.

“Kwa hiyo, kupitia mradi huu tumehakikisha kwamba huduma za uzazi wa mpango zinafanikiwa na zinapatikana kwa wakati, na kuwafikia vijana wanawake lakini bila kuwaacha nyuma watu wenye ulemavu,” amesema Dk Bright.

Hata hivyo, amesema licha ya kuufunga mradi huo, bado kazi haijakamilika, kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *