
Mbeya. Vijana mkoani Mbeya wamewasilisha mapendekezo manane wanayodhani yanaweza kusaidia kuimarisha amani na utulivu nchini, huku Serikali ikiahidi kuyafanyia kazi kwa kuzingatia uwezo wa utekelezaji wa muda mfupi, wa kati na mrefu.
Baadhi ya mapendekezo hayo yanahusu uwajibikaji, usawa, uwazi, usimamizi thabiti, ushirikishwaji na utekelezaji wa maamuzi, huku wakisisitiza pia kuanzishwa kwa mabaraza ya vijana kuanzia ngazi ya jamii ili kuongeza uwakilishi wa moja kwa moja katika mifumo ya maamuzi ya Serikali.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa leo Jumamosi Juni 27, 2026 katika warsha ya siku mbili inayozungumzia mradi wa Dumisha Amani, unaofadhiliwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Amani na Maendeleo (UNPDF) kupitia Mfuko Mdogo wa Amani na Usalama wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, unalenga kufikia mikoa minne katika awamu ya kwanza.
Akizungumza katika warsha hiyo, mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mbeya, Jackson Kaaya amesema kuimarika kwa amani kunahitaji kuzingatiwa kwa misingi ya sheria, usawa wa kijinsia, uwajibikaji na utekelezaji wa maamuzi.
“Tunapaswa kuzingatia sheria na misingi iliyowekwa, na yale yanayosimamiwa yatekelezwe kwa haki na usawa bila upendeleo. Vijana pia wanapaswa kujitoa kushiriki kabla ya kushirikishwa,” amesema Kaaya.
Naye Sylivester Julius amesema uimarishaji wa amani na usalama unahitaji maboresho ya mifumo ya usimamizi, uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa vijana katika maamuzi ya kitaifa.
“Vijana kama nguvu kazi ya taifa wanapaswa kuwa sehemu ya maamuzi na kuonesha mwamko katika masuala ya kijamii kuelekea Dira ya Taifa 2050,” amesema Julius.
Kwa upande wake, Mariana Mwampinde amesisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na kuwataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa kujenga badala ya kubomoa.
“Vijana wasiwe sehemu ya kusambaza au kuchochea taarifa mitandaoni, bali wawe mfano wa kujenga taifa na kuondoa matabaka kwa kushirikiana,” amesema.
Akizungumzia mapendekezo hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa amesema Serikali itayafanyia kazi kwa kuzingatia muda na vipaumbele vya utekelezaji.
Amesema warsha hiyo imewezesha kubaini changamoto mbalimbali na kujadili pia fursa za kiuchumi zinazoweza kuwanufaisha vijana, huku akiahidi kuwasilisha maoni hayo kwenye mamlaka husika.
“Tumejifunza kuwasilisha changamoto bila vurugu, kujadili fursa na namna ya kuzifikia ili kujiinua kiuchumi. Kama kiunganishi cha Serikali na wananchi nitahakikisha mapendekezo haya yanafikishwa,” amesema.
Mchambuzi wa mradi wa Dumisha Amani, Edmund Mbigili amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha amani kwa ajili ya maendeleo endelevu nchini Tanzania, ukilenga awamu ya kwanza kufikia mikoa minne.
Amesema ushiriki wa vijana umeonesha mwamko mkubwa katika kuhamasisha amani na kushiriki katika utatuzi wa migogoro kuanzia ngazi za jamii hadi kitaifa.
“Mawazo ya vijana yanaonesha dhamira ya kuchochea amani na maendeleo. Ndiyo maana tumewashirikisha makundi mbalimbali ili kupata picha halisi ya changamoto na suluhisho,” amesema Mbigili.
Warsha hiyo imeshirikisha makundi ya waendesha bodaboda, wanafunzi, mashirika yasiyo ya kiserikali, watengeneza maudhui mitandaoni pamoja na wajasiriamali wadogo ikilenga kujengeana uwezo, kubaini changamoto na kutoa mapendekezo ya kijamii na kiuchumi yatakayosaidia kudumisha amani nchini.