Dar es Salaam. Kampuni ya Perseus Mining imesema imeingiza zaidi ya Sh457.7 bilioni katika uchumi wa Tanzania kupitia maandalizi ya mradi wa dhahabu wa Nyanzaga, hata kabla ya kuanza uzalishaji wa kibiashara unaotarajiwa kuanza katika robo ya kwanza ya mwaka 2027.

Takwimu zilizotolewa na kampuni hiyo zinaonesha kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2026, mradi huo umetumia Sh371.6 bilioni kununua bidhaa na huduma kutoka kwa wazabuni wa Kitanzania, kulipa Serikali Sh60.7 bilioni kama kodi na tozo mbalimbali, huku Sh25.1 bilioni zikielekezwa kwenye mishahara na stahiki za wafanyakazi.

Aidha, zaidi ya Sh305 milioni zimetumika kufadhili miradi ya maendeleo ya jamii inayozunguka mgodi huo uliopo Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Meneja wa Sotta Mining Corporation Limited, kampuni tanzu ya Perseus Mining inayotekeleza mradi huo, Isaac Lupokela, amesema manufaa ya kiuchumi na kijamii ya mradi huo tayari yanaonekana, licha ya uzalishaji wa dhahabu kutokuwa umeanza.

“Kama sehemu ya dhamira yetu ya kuendesha uchimbaji madini kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu, tumejikita katika kujenga thamani ya kudumu kwa jamii zinazotuzunguka na kwa uchumi wa Tanzania. Manufaa ya mradi wa Nyanzaga yanaanza kuonekana hata kabla ya uzalishaji wa dhahabu kuanza,” amesema.

Kwa mujibu wa Lupokela, shughuli za ujenzi wa mgodi huo zimezalisha ajira kwa zaidi ya watu 3,600, wakiwemo wafanyakazi wa moja kwa moja 281, huku wengi wao wakiwa Watanzania na sehemu kubwa wakitoka katika jamii zinazouzunguka mradi.

Kampuni imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kutoa nafasi 202 za mafunzo ndani ya mwaka mmoja uliopita na kuanzisha Kamati ya Ajira ya Jamii ili kuongeza uwazi na ushiriki wa wananchi wa maeneo ya mradi katika fursa za ajira.

Mbali na ajira, kampuni hiyo imekamilisha miradi ya maji katika vijiji vya Sotta Mashariki na Sotta Magharibi, huku ikiendelea na kampeni za uhamasishaji kuhusu afya, usalama kazini na utunzaji wa mazingira.

Pia, inaendelea na ujenzi wa shule mpya ya msingi kuchukua nafasi ya iliyokuwapo, shule nyingine mpya, zahanati pamoja na Barabara ya Mchepuko ya Ngoma (Ngoma Bypass Road), ambayo inatarajiwa kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara na wakazi wa eneo hilo.

Mradi wa Nyanzaga unakadiriwa kuwa na akiba ya takribani wakia milioni nne za dhahabu na unatarajiwa kuzalisha kwa angalau miaka 16 baada ya kuanza rasmi uzalishaji wa kibiashara.

Kwa sasa, ujenzi wa mgodi huo umefikia takribani asilimia 50 na umegharimu Dola milioni 250 za Marekani. Perseus Mining inamiliki asilimia 80 ya mradi huo, huku Serikali ya Tanzania ikimiliki asilimia 20 kupitia ubia wake katika Sotta Mining Corporation Limited.

Kampuni hiyo inaeleza kuwa mradi unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali, kuzalisha ajira za kudumu na kufungua fursa zaidi za biashara, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayotambua sekta ya madini kuwa miongoni mwa nguzo za kukuza uchumi wa nchi.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Perseus Mining, Rick Menell, akizungumzia mradi huo, alisisitiza wajibu wa kampuni hiyo kusimamia rasilimali za Taifa kwa uadilifu.

“Rasilimali hizi ni mali ya Tanzania. Tunajiona kuwa wasimamizi wake kwa niaba ya Taifa, hivyo tunahakikisha zinatumika kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,” alisema.

Menell alisema kampuni ina mpango wa kuufanya mradi wa Nyanzaga kuwa kituo cha mafunzo ya kiufundi kitakachochangia kuzalisha wataalamu wa baadaye katika sekta ya madini.

Mmoja wa wakazi wa Sengerema, Frank Masumbuko, alisema miradi mbalimbali huja na maendeleo, ikiwemo ya afya, maji na barabara, huku akiomba hilo lifanyike kwa viwango.

“Wananchi wanapenda uwekezaji mbalimbali, na tunapenda zaidi tunapoona tunanufaika. Kama tunapata ajira, shule na zahanati zinajengwa, haya ni matunda makubwa, na tunawaomba wawekezaji kuwazingatia wananchi wanaozunguka mgodi,” alisema Masumbuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *