Moshi. Wafanyabiashara wa pembezoni mwa barabara katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamehamishwa baada ya Serikali kupiga marufuku biashara katika maeneo hayo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia ajali ya lori aina ya Mitsubishi Canter (Fuso) lililofeli breki, kuacha njia na kuvamia vibanda vya wafanyabiashara pamoja na watembea kwa miguu, na kusababisha majeraha kwa watu kadhaa na uharibifu wa mali katika tukio lililotokea jana, Jumamosi Juni 27, 2026.

Agizo hilo limetolewa leo, Jumapili Juni 28, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliyesema wafanyabiashara wanaopanga bidhaa pembezoni mwa barabara wanajiweka kwenye hatari, hivyo wanapaswa kuhamia katika masoko yaliyotengwa na Serikali badala ya kufuata wateja barabarani.

“Tuendelee kuwahimiza na kuwataka wafanyabiashara wetu kutokupanga biashara zao katika maeneo ya barabarani. Waingie katika maeneo tuliyoyatenga. Waache kutoka ndani ya soko kwenda barabarani kwa sababu si salama,” amesema.

Mnzava amesema endapo maeneo yaliyopo ndani ya masoko yatajaa, Serikali itaweka utaratibu na kutoa maelekezo ya maeneo mengine salama yatakayoweza kutumika kwa ajili ya biashara.

Katika ajali hiyo iliyotokea saa mbili kasoro asubuhi, lori hilo lilikuwa likitokea eneo la Msikiti wa Riadha kuelekea Soko la Manyema kabla ya kupoteza mwelekeo na kusababisha majeraha pamoja na uharibifu mkubwa wa mali.

Kwa mujibu wa Mnzava, watu sita walijeruhiwa, wakiwemo wanawake watano na mwanaume mmoja, na wote walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi kwa msaada wa wananchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema polisi wanalishikilia lori hilo linalomilikiwa na Luchmen Suleiman Msoffe, huku wakiendelea kumsaka dereva aliyekimbia baada ya ajali.

Amesema taarifa rasmi za polisi zinaonyesha majeruhi waliorekodiwa ni watatu ambao ni Sikudhani Nuru Msangi (38), mfanyabiashara na mkazi wa Mabogini; Elinipa Matemba (75), mkazi wa Majengo; na Daniel Lazaro Lemeru (37), mkazi wa Arusha.

“Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari kwenye eneo lenye mkusanyiko wa watu na watumiaji wengine wa barabara, ambapo alikimbia baada ya ajali hiyo,” amesema Maigwa.

Baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa masoko wameunga mkono agizo hilo, huku wakisema changamoto ya kukosa wateja ndani ya masoko ndiyo inayowalazimu kwenda kupanga bidhaa pembezoni mwa barabara.

Amina Juma, mfanyabiashara wa mbogamboga katika Soko la Manyema, amesema wanafahamu hatari ya kufanya biashara karibu na barabara, lakini hulazimika kufanya hivyo kwa kuwa wateja wengi hununua bidhaa zilizo nje ya soko.

“Sisi wenyewe tunajua ni hatari kukaa karibu na barabara, lakini ukiingia ndani ya soko wateja hawaingii kabisa. Onyo la hili ni zuri na lina lengo la kulinda maisha yetu, lakini tunaomba Serikali ihakikishe kila mtu anaingia ndani ya soko bila upendeleo,” amesema.

Naye dereva wa bajaji, John Mushi, amesema msongamano wa wafanyabiashara barabarani umeendelea kuwa kero kwa watumiaji wa vyombo vya moto, akitaka operesheni hiyo isifanyike Manyema pekee, bali pia katika eneo la Mbuyuni ili kuzuia ajali zinazoweza kujitokeza baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *