Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Bara, Benson Kigaila amesema hatima ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu kuhusu kukataliwa au kutokataliwa na wajumbe itafahamika baada ya mchakato wa ndani wa chama kukamilika.

Amesema hoja hiyo bado ipo kwenye vikao vya chama na wajumbe wa Halmashauri Kuu ndiyo wenye mamlaka ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Kutokana na hali hiyo, amesema si busara kuzungumzia suala hilo kana kwamba tayari limehitimishwa.

“Baada ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokamilika jioni ya leo, kila jambo litawekwa wazi kwa umma,” amesema Kigaila.

Jana Jumatatu, Juni 29, 2026, taarifa zilizozua mjadala mkubwa mitandaoni zilidai baadhi ya wajumbe wa sekretarieti na Kamati Kuu ya Chaumma walipiga kura ya kutokuwa na imani na Salum Mwalimu, wakimtuhumu kwa kufanya uamuzi binafsi bila kufuata utaratibu wa chama.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, waraka uliosainiwa na wajumbe waliopiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu uliwasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana na kuhitimishwa saa tano usiku.

Lengo la kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe

ilikuwa kuandaa hoja zitakazowasilishwa mbele ya Halmashauri Kuu, ambayo leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho kwa kupiga kura ya ndiyo au hapana.

Vyanzo vya ndani vya chama vinaeleza miongoni mwa sababu zilizochangia Mwalimu kukataliwa na wajumbe ni madai kwamba amekuwa akijiamulia mambo, ikiwemo kutoa maoni binafsi na kuyawasilisha kama misimamo rasmi ya vikao vya chama.

Baadhi ya maoni yanayotajwa kutokuwa msimamo wa Chaumma  na kujikuta akikaliwa kooni na wajumbe ni pamoja na kuipongeza na kuisifia Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29, 2025. Msimamo huo unadaiwa kuwagawa wanachama wa chama hicho katika makundi mawili.

Sababu nyingine inayotajwa ni madai ya ubadhirifu wa fedha, hoja ambayo  awali iliwahi kujadiliwa katika kikao kati ya uongozi wa chama na makatibu wa mikoa mapema mwaka huu kwamba walipunjwa fedha za mchakato wa uchaguzi mkuu wa Serikali mwaka 2025.

Leo, Jumanne Juni 30, 2026, Mwananchi ilizungumza na Kigaila, ambaye jana  hakuzungumza kutokana na kuongoza kikao baada ya Mwalimu kudaiwa kuingia mitini kwenye kikao hicho kufuatia kutakiwa kujitetea dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Akizungumzia suala hilo, Kigaila amesema mchakato bado haujakamilika, hivyo si sahihi kutoa hitimisho kabla Halmashauri Kuu haijafanya uamuzi wake.

“Hoja unayoieleza bado ipo kwenye vikao vya chama na mchakato wake haujakamilika. Si busara kuizungumzia kwa undani kwa sababu Halmashauri Kuu ambayo ndiyo yenye uamuzi wa mwisho, bado haijapiga kura ya kuridhia au kukataa,” amesema.

Amesema kutokana na uzito wa uamuzi wa Halmashauri Kuu, matokeo ya mchakato huo yatawekwa hadharani baada ya kikao hicho kumalizika jioni ya leo.

“Jioni ya leo baada ya kikao cha Halmashauri Kuu tutasema kama Mwalimu amekataliwa au hajakataliwa, ikiwa amekataliwa tutakuja na suluhu, kwa sasa tuache mchakato wa ndani wa chama uendelee na tuheshimu taratibu zake,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu taarifa zinazomtaja kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi wadhifa wa Katibu Mkuu endapo Mwalimu ataondolewa, Kigaila amekataa kuzungumzia suala hilo.

“Siwezi kusema chochote kwa sasa. Mchakato wa vikao vya ndani bado haujakamilika. Naomba tuheshimu taratibu za chama; ukweli wote utajulikana baada ya mchakato kukamilika,” amesema Kigaila.

Mwananchi inaendelea kumsaka Mwalimu kuhusu ukweli wa madai ya kukataliwa kwake kila akitafutwa kwa simu haipatikani.

Vikao vya Halmashauri Kuu vinatarajiwa kuanza saa tano asubuhi ya leo, Makao makuu ya chama hicho Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam na kwa sasa bado wajumbe wanawasili kujiandaa na kikao hicho cha siku moja.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *