Dar es Salaam. Mashindano ya NCBA Golf Series 2026 yameanza rasmi kwa kishindo, yakikusanya pamoja wachezaji wa gofu, viongozi wa biashara, wafanyabiashara, wadau na wateja katika tukio lililoonesha kuwa mchezo wa gofu unaweza kuwa zaidi ya mashindano ni jukwaa la kujenga mahusiano, kuibua fursa na kuendeleza maendeleo ya kiuchumi.

Kwa NCBA Bank Tanzania, Golf Series si tukio la michezo pekee. Ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya benki ya ‘Banking on Belief. Empowering Ambitions’, inayolenga kuwawezesha watu, biashara na jamii kufikia ndoto na malengo yao.

Akizungumza mwishoni mwa wiki kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Bank Tanzania, Rahim Suleiman, Mkuu wa Kitengo cha masoko ya kimataifa (Global Markets), alisema mashindano hayo yanaonesha namna benki inavyoendelea kuwekeza katika majukwaa yanayowaunganisha watu na kufungua milango ya ushirikiano na ukuaji wa biashara.

“Sisi NCBA tunaamini benki si mahali pa kuhifadhi fedha pekee, bali ni mshirika wa maendeleo. Tunaamini katika ndoto za wateja wetu na tunajenga mazingira yanayowawezesha kuzitimiza. Golf Series ni mojawapo ya majukwaa yanayowaleta pamoja viongozi wa biashara, wafanyabiashara na wadau mbalimbali ili kujenga mahusiano yatakayozalisha fursa mpya za maendeleo,” alisema Suleiman.

Alisema falsafa hiyo ndiyo msingi wa kampeni ya benki ya Ndoto Zako, Hatua Zetu, inayodhihirisha dhamira ya NCBA ya kusimama bega kwa bega na wateja wake katika safari yao ya kufikia mafanikio.

Kupitia huduma zake za Asset Finance, NCBA imeendelea kusaidia wafanyabiashara na wajasiriamali kupata mitaji ya vifaa, mashine na magari yanayowawezesha kuongeza uzalishaji, kupanua biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mbali na huduma za kifedha, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika maendeleo ya jamii kupitia programu mbalimbali za uendelevu. Hizi ni pamoja na programu ya maendeleo ya vijana wa mchezo wa gofu (Junior Golf Development Programme), ambapo hutoa vifaa vya mchezo, mafunzo na kusaidia ustawi wa vijana wanaojifunza gofu, pamoja na miradi ya upandaji miti inayolenga kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Mashindano ya mwaka huu yalianza kwa ushindani mkubwa huku Mwizani Julius akiibuka mshindi wa jumla kwa upande wa wanaume na Letisia Kapalia kutwaa ushindi wa jumla kwa upande wa wanawake, wakionesha kiwango cha juu cha ushindani na umahiri.

Ushindi wao unaashiria mwanzo wa safari ya kuelekea fainali za NCBA Golf Series, ambapo baada ya mashindano mengine mawili ya mchujo, wachezaji bora kutoka Tanzania watapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika fainali za kikanda zitakazofanyika jijini Nairobi, Kenya, pamoja na mabingwa kutoka Uganda, Rwanda na Kenya.

Kwa miaka kadhaa sasa, NCBA Golf Series imeendelea kujijengea heshima kama moja ya majukwaa makubwa zaidi ya gofu na mitandao ya biashara Afrika Mashariki. Mbali na ushindani wa mchezo, mashindano haya yanawawezesha wadau kujenga mahusiano mapya, kubadilishana mawazo na kuanzisha ushirikiano unaochochea ukuaji wa biashara.

Suleiman alisema mafanikio ya NCBA hayaishii katika utoaji wa huduma za kifedha pekee, bali yanapimwa pia kwa mchango wake katika kuwawezesha watu na jamii kufikia malengo yao.

“Tunapoizungumza kaulimbiu yetu ya Banking on Belief. Empowering Ambitions, tunamaanisha kuamini katika uwezo wa watu na kuwapa fursa za kufanikiwa. Tunafanya hivyo kupitia huduma zetu za kifedha, uwekezaji katika michezo, programu za maendeleo ya vijana na miradi ya uendelevu inayogusa maisha ya Watanzania wengi,” alisisitiza.

Mashindano haya yataendelea kupitia raundi mbili zaidi za mchujo kabla ya kupata wawakilishi wa Tanzania watakaoshiriki fainali za Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *