Mwanza. Wakuu wa idara katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kufanya tathmini maalumu ya madeni ya walimu kufuatia kuongezeka kwa walimu wanaokabiliwa na mzigo mkubwa wa mikopo unaoathiri utendaji wao kazini.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda baada ya kubaini kuwa walimu zaidi ya 254 wanadaiwa mikopo inayozidi uwezo wao wa kulipa, hali inayosababisha msongo wa mawazo, utoro kazini na kushuka kwa ubora wa elimu.
Akizungumza katika kikao maalumu cha kusikiliza utekelezaji wa hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) June 29, 2026, Mtanda amesema baadhi ya walimu wamejikuta wakikopa kwenye taasisi zisizo rasmi kwa riba kubwa.
Amesema mikopo hiyo inakuwa kinyume na taratibu za Serikali zinazotaka mtumishi kubaki na angalau theluthi moja ya mshahara wake kwa matumizi ya msingi.
“Idara ya elimu lazima ijue hali halisi ya walimu wake….fanyeni tathmini ya kina ili tuweze kupata suluhisho la kudumu,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Tutakaa na hawa walimu pamoja na taasisi zinazowakopesha. Kama wamekopesha kinyume na utaratibu, hatua zitachukuliwa ikiwemo kufuta riba ili kurejesha mikopo katika kiwango kinacholipika kisheria.”
Meya wa Manispaa ya Ilemela, Sara Ngw’ahni akizungumza kwenye baraza maalumu la kusikiliza utekelezaji wa hoja za CAG .
Aidha, amefichua kuwepo kwa matukio ya udanganyifu ambapo baadhi ya walimu 16 wa wilayani Nyamagana walilazimika kufoji nyaraka, kujifanya watumishi wa sekta ya afya na kwenda kukopa mkoani Simiyu, jambo lililochangia kuongezeka kwa madeni yenye riba kubwa hadi kufikia asilimia 150.
Mwalimu wa shule ya msingi (jina limehifadhiwa) amesema hali ya madeni imewalazimu baadhi ya walimu kubuni vyanzo vya ziada vya mapato ili kujikimu.
“Tunafanya mambo mengi ya ziada shuleni ili kujiingizia kipato, ikiwemo kuuza vitafunwa na kuanzisha masomo ya ziada…mikopo inatutesa sana walimu, tunalazimika kukopa huku na kule, wakati mwingine mkopo hatuufanyii kitu cha maana zaidi ya kulipa madeni ya nyuma yanayotusumbua,” amesema.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana ameagiza Manispaa ya Ilemela na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuundwa kwa timu maalumu itakayoshughulikia hoja za CAG, ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi wa kujibu hoja hizo.
Elikana amesema menejimenti inapaswa kuwasilisha muundo wa timu hiyo ndani ya siku 14, huku akisisitiza kuwa hoja zinazojirudia kila mwaka lazima zikomeshwe kwa kuchukua hatua stahiki.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana akitoa maelekezo ya kuundwa kwa kamati za kujibu hoja za CAG wakati wa kikao maalumu cha kusikiliza utekelezaji wa hoja hizo.
“Hatutaki kuona hoja zilezile zinajirudia kila mwaka…uwajibikaji lazima uonekane,” amesisitiza.
Kuhusu mapato, Mtanda ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani Manispaa ya Ilemela akisisitiza haja ya kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo itakayobadili taswira ya halmashauri.
“Tunataka tukija hapa mwakani mtwambie miradi mikubwa yenye kuleta taswira kubwa hapa Ilemela inayotokana na mapato ya ndani ni miradi gani,”amesema.
Wakati huohuo, Mtanda amepongeza wananchi 107 kulipwa fidia ya Sh194 milioni ya ardhi waliyoangaikia kwa miaka saba.