Takriban miezi mitatu imepita tangu kumalizika kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel katika ardhi ya Iran, lakini kila siku, na kufuatia kuchapishwa nyaraka mpya na picha pamoja na simulizi tofauti, viwango vipya vya jinai za wavamizi hao vinafichuliwa.

Kile ambacho hakikuonekana wakati wa siku za vita kati ya moshi, moto na simulizi za awali, leo, ripoti za nyanjani na ushahidi wa mashuhuda, unatoa picha tofauti kabisa kuhusu mashambulizi hayo. Jinai ya Lamerd ni mojawapo ya kesi za kushtua sana. Shambulio ambalo, ikiwa matokeo ya ripoti ya uchunguzi ya chombo cha habari cha Uingereza “Middle East Eye” yatachukuliwa kuwa msingi wa maamuzi, ni mfano wa wazi wa matumizi ya mfumo mpya wa silaha dhidi ya eneo la makazi ya raia.

Ripoti mpya ya “Middle East Eye”, iliyotayarishwa kwa msingi wa picha za nyanjani, ripoti za matibabu, ushahidi wa mashuhuda na uchunguzi wa eneo la tukio, inafichua ukatili ambao ulifanywa na mfumo wa kombora la Precision Strike lililotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin na ambalo lilitumika kwa mara ya kwanza katika historia yake ya operesheni dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makombora manne yalitumika kulipua sio kambi ya kijeshi au kituo cha kimkakati, bali mitaa miwili ya makazi katika mji wa Lamerd ulioko kusini mwa Iran, ambapo shule, ukumbi wa mazoezi, uwanja wa mpira, nyumba za makazi na maduka yalilipuliwa kinyama, na watoto waliokuwa wakifanya mazoezi ya mpira wa wavu na wa miguu kuuliwa kikatili. Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari, kila kombora lilibeba takriban risasi 180,000 za tungsten, na risasi nyingine 720,000 kutapakaa kila mahali katika eneo hilo. Ripoti ya uchunguzi ya gazeti la New York Times pia imewanukuu wataalamu wa silaha wakisema kuwa namna ya milipuko angani na taathira zilizoachwa nyuma zinaoana kabisa na sifa za mfumo huo wa makombora. Ikiwa matokeo haya yatathibitishwa na uchunguzi huru, Lamerd itakuwa mfano wa kwanza uliorekodiwa wa matumizi ya kioperesheni ya mfumo huu dhidi ya eneo la kiraia.

Taathira za kinyama za shambulio hilo ni za kushangaza na kutisha zaidi. Katika shambulio hilo, raia 21 wakiwemo watoto sita waliuawa shahidi na zaidi ya watu 150 wakajeruhiwa. Miongoni mwa waliouawa shahidi ni msichana wa miaka miwili ambaye alikufa kutokana na kupigwa na vipande vya risasi alipokuwa akicheza uwanjani. Msichana mwenye umri wa miaka 15 pia alipoteza kabisa uwezo wa kuona, mwanafunzi mwingine akapoteza uwezo wa kuongea, na watoto kadhaa wakalemazwa kabisa na vipande vya risasi. Wengine walipoteza uwezo wao wa kutembea kutokana na kusagwa mifupa na kukatwa mishipa ya miguu. Hizi sio nambari na takwimu tu. Kila mmoja wa wahanga hawa ana maisha, mustakbali wa baadaye, na familia ya kushughulikia ambapo sasa atabeba taathira za shambulio hilo katika maisha yake yote. Kinachotofautisha ripoti hii na simulizi nyingine za vita ni aina ya majeraha yaliyosababishwa. Moussa Mousavi, daktari wa upasuaji katika Hospitali ya Lamerd, anasisitiza kwamba aina ya majeraha yanayosababishwa na risasi za tungsten kimsingi ni tofauti na yale aliyoyaona wakati wa vita vya Iran na Iraq. Risasi hizi si tu hunasa mwilini, bali pia huingia kwenye mifumo ya tishu, na katika baadhi ya kesi kulipukia ndani ya viungo vya ndani ya mwili, na hatimaye kuacha humo uharibifu mkubwa ambapo ni wazi kuwa lengo sio kuua, bali ni kuwasababishia wahanga ulemavu wa kudumu na mateso makali.

Sehemu muhimu zaidi ya ripoti hii ni kutokuwepo ishara yoyote ya kijeshi katika maeneo yaliyoshambuliwa. Middle East Eye inasisitiza kwamba uchunguzi wa nyanjani uliofanywa na vyombo vya habari haujaonyesha uwepo wa aina yoyote ya vituo vya kijeshi au kistratijia katika eneo hilo na kwamba wahanga wote walikuwa raia wa kawaida. Hii ni katika hali ambayo Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) siku chache tu baada ya shambulio hilo, ilieleza matumizi ya kwanza kabisa ya kivita ya makombora hayo dhidi ya Iran kuwa mafanikio ya kijeshi. Kufanana majeraha yaliyorekodiwa huko Lamerd na kuchapishwa ripoti za utumiwaji wa mabomu sawa na hayo na utawala wa Israel dhidi ya raia huko Gaza kunasisitiza haja ya kufanyika uchunguzi wa kina zaidi kuhusu muundo wa matumizi ya aina hii ya silaha. Swali linaibuka hapa kuwa je, silaha hizi zinazodaiwa kuwa zenye “usahihi wa hali ya juu” zimekuwa njia ya kuleta madhara makubwa zaidi ya kimwili na kisaikolojia kwa raia wa kawaida? Kutofanyika uchunguzi wowote huru wa kimataifa kunazua maswali mazito kuhusu uzembe unaofanywa na taasisi husika katika kushughulikia suala hili muhimu. Leo, Lamerd si jina la mji tu; inawakilisha majeraha ambayo bado yako kwenye miili ya makumi ya watoto na mamia ya waliojeruhiwa, na ndani ya maisha ya familia zilizofiwa. Vifo vya watoto sita—akiwemo binti mdogo wa umri wa miaka miwili aliyekuwa akicheza uani mwa nyumba yao—na mamia ya waliojeruhiwa, ambao baadhi yao wataishi na ulemavu maisha yao yote, ni ukumbusho kamili kwamba matokeo ya vita yanavuka na kuenea zaidi ya siku za mapigano.

Ingawa imechapishwa kwa kuchelewa, lakini ripoti ya “Middle East Eye” ni dirisha la kushuhudia ukubwa halisi wa mojawapo ya mashambulizi ya kuhuzunisha zaidi dhidi ya raia wakati wa vita vya karibuni. Kufichuliwa ukweli, kuwajibishwa watenda-jinai, kufanywa uchunguzi huru, na kunukuliwa kwa usahihi matukio haya ni matakwa yasiyopingwa — sio kwa watu wa Lamerd pekee bali kwa ajili ya kulinda itibari ya sheria za kimataifa na kuzuia kukaririwa majanga kama hayo katika siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *