• Mahakama Kuu imeamua kuwa wasichana wanane wanaohusishwa na moto wa Utumishi Girls Academy watatambuliwa kama watoto, si washukiwa wala washtakiwa, wakati wa kesi
  • Jaji Diana Kavetsa alitangaza kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, mahakama itabadilishwa na kuwa Mahakama ya Watoto, akisisitiza kuwa haki zao za kikatiba kama watoto zitalindwa licha ya uzito wa mashtaka yanayowakabili
  • Akizingatia uzito wa mashtaka pamoja na ukweli kwamba wasichana hao ni watoto, Kavetsa alisema kesi hiyo itaamuliwa kwa kuzingatia ushahidi na sheria, si maoni ya umma

Mahakama Kuu ya Kibera imeagiza kuwa wasichana wanane wanaohusishwa na shambulio la uchomaji moto katika Utumishi Girls Academy lililosababisha vifo vya wanafunzi 16 hawataitwa washukiwa wala washtakiwa wakati wa mwenendo wa kesi.

Watuhumiwa wa moto Utumishi Academy.
Watuhumiwa wa moto wa Utumishi Academy wakifikishwa mahakamani. Picha: Kihuria Ndorongo.
Source: Facebook

Kwa mujibu wa Jaji Diana Kavetsa anayesikiliza kesi hiyo, hadhi ya wasichana hao kama watoto lazima ilindwe katika kipindi chote cha kesi, akitangaza kuwa watajulikana kama “watoto wanaohusika katika shauri”.

Wasichana hao wanane walifika mahakamani Jumanne, Julai 1, kwa ajili ya kusomewa mashtaka kuhusiana na moto huo wa kusikitisha uliotokea alfajiri ya Mei 28.

Pia soma

Magazeti ya Kenya, Julai 1: NTSA sasa yafyata mkia kuhusu sheria ya ukaguzi wa lazima wa magari

Baada ya wasichana hao kufikishwa mbele yake, Kavetsa alisisitiza kuwa istilahi zinazotumiwa kuwahusu zitabadilishwa ipasavyo.

“Hakuna mtu atakayewaita washtakiwa. Hatuwezi kuwa na washtakiwa hapa. Hawa ni watoto,” aliiambia mahakama, akielekeza kuwa kwa kipindi kilichobaki cha kesi hiyo wataitwa watoto wanaohusika katika shauri.

Aidha, mahakama hiyo itabadilishwa rasmi kuwa mazingira yanayofaa na salama kwa watoto ili kushughulikia kesi hiyo kwa kuzingatia hitaji la kufungua jalada maalumu la watoto wanaokabiliwa na tuhuma za uhalifu.

“Kwa hivyo, mahakama itajigeuza wakati fulani kuwa Mahakama ya Watoto,” alisema.

Wakati huohuo, jaji huyo alitangaza kuwa ni Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na mawakili wanaowawakilisha watoto hao pekee watakaoruhusiwa kuwa ndani ya mahakama wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Wakati huo huo, alikiri kuwa janga hilo limewaumiza sana Wakenya, akieleza kuwa shule hiyo ilibadilika mara moja kutoka kuwa mahali pa kujifunzia hadi kuwa ishara ya maombolezo ya kitaifa.

Kavetsa alisema taifa linastahili kupata majibu na haki, lakini akaonya dhidi ya kuruhusu hisia za umma kuathiri mchakato wa haki.

Alisisitiza kuwa kesi hiyo itaamuliwa kwa kuzingatia ushahidi unaokubalika mahakamani na sheria husika pekee.

Pia soma

Davis Lichuma: Familia yazungumza kwa uchungu baada ya mwanaharakati kupatikana lakini hajitambui

“Haki haiwezi kutolewa kwa misingi ya hasira za umma, wala haiwezi kuamuliwa kwa maoni ya mitandao ya kijamii au maoni ya wananchi,” alisema.

Jaji huyo alibainisha kuwa watoto hao wanakabiliwa na shtaka zito zaidi la jinai linalotambuliwa chini ya sheria za Kenya, lakini akasisitiza kuwa hali hiyo haiondoi haki zao za kikatiba kama watoto.

“Uzito wa madai yanayowakabili hauondoi haki zao za kikatiba. Vivyo hivyo, ukweli kwamba wao ni watoto haupunguzi uzito wa maisha yaliyopotea,” alisema, akiongeza kuwa jukumu la mahakama ni kusawazisha hali hizo mbili bila kuathiri upande wowote.

Aliongeza kuwa maslahi makubwa ya umma kuhusu kesi hiyo yamemfanya kuweka mapema mwongozo wa jinsi kesi hiyo itakavyoendeshwa.

Jaji huyo alisema mfumo wa kina wa kuongoza mwenendo wa kesi utawekwa haraka iwezekanavyo kutokana na uangalizi mkubwa unaoizunguka kesi hiyo.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *