
Dunia inashuhudia mshikamano wa kipekee kufuatia taarifa kwamba wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 90, pamoja na viongozi wa kidini, wasomi, na watu mashuhuri kutoka kila pembe ya dunia, wanatarajiwa kushiriki katika shughuli za mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran anayeshughulikia masuala ya usalama, Ali Akbar Pourjamshidian, ambaye pia ni katibu wa kamati ya maandalizi ya mazishi hayo, amethibitisha kuwa zaidi ya nchi 30 tayari zimewasilisha maombi rasmi ya kutuma ujumbe wa ngazi ya juu kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
Pourjamshidian amesema kuwa mazishi ya Kiongozi Shahidi yaliakhirishwa ili kutoa nafasi ya kutosha ya kupanga tukio hili kubwa la kitaifa na kimataifa, kwa kuzingatia mazingira ya hivi karibuni nchini.
Amesema kulingana na maelekezo ya ofisi ya Kiongozi Shahidi na mwongozo wa Kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyed Mojtaba Khamenei, shughuli hizo zitaendelea kwa siku kadhaa. Aidha amedokeza kuwa mipango yote inasimamiwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Ofisi ya Kiongozi, na Kamati Maaulumu ya Kitaifa iliyo chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mohammad Reza Aref.
Pourjamshidian amebainisha kuwa mamlaka husika zimetangaza mapumziko ya umma ili kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika hafla hizo za kihistoria, ambapo mkoa wa Tehran utakuwa na mapumziko kuanzia Julai 4 hadi 5, huku siku ya Julai 6 ikitangazwa kuwa sikukuu ya kitaifa nchi nzima kwa ajili ya msafara mkuu wa mazishi jijini Tehran. Vilevile, mkoa wa Qom utakuwa na mapumziko siku ya Julai 7 wakati msafara wa mazishi utakapofika mkaoni humo. Halikadhalika mkoa wa Khorasan Razavi utaungana na ratiba hiyo siku ya Julai 9 ili kurahisisha utaratibu wa kutoa heshima za mwisho kwa Kiongozi Shahidi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa mnamo Julai 8 mwili wa Kiongozi Shahidi utapelekwa nchini Iraq, ambapo mapokezi rasmi yatafanyika katika uwanja wa ndege wa Baghdad au Najaf, yakifuatiwa na maandamano na ibada maalum katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.
Pourjamshidian amesisitiza kuwa shughuli hizi ni kielelezo cha nguvu ya taifa la Iran, na zinalenga kuimarisha umoja miongoni mwa wananchi wa Iran na ulimwengu mpana wa Kiislamu. Aidha amesema ni fursa pia ya kufanya upya ahadi ya utiifu kwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha amesema: “Tunatarajia ushiriki mpana kutoka nchi za Kiislamu, zikiwemo Iraq, Pakistan, Afghanistan, na mataifa mengine jirani, jambo litakalozidi kuimarisha mshikamano wa Waislamu.”
Zaidi ya waandishi wa habari 300 wa kigeni wamesajiliwa kuripoti tukio hili. Mamlaka imehakikisha kuwa hakutakuwa na vikwazo vyovyote vya mtandao wakati wa hafla hizo, na namba maalum ya dharura imewekwa ili kutoa msaada na taarifa kwa washiriki.