
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimeripoti kutokea vurugu na mapigano ndani ya Bunge la utawala huo (Knesset), kufuatia kufutwa sheria iliyokuwa inahusu wafungwa wa Kipalestina.
Mtandao wa Kan wa utawala wa Kizayuni uliripoti kwamba, wakati wa mjadala kuhusu kufutwa sheria iliyokuwa ikizuia wajumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuwatembelea wafungwa wa Kipalestina, kulitokea vurugu na mapigano makali ndani ya Bunge la utawala huo (Knesset).
Kwa upande mwingine, gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliandika kuwa muswada wa sheria uliokuwa umewasilishwa katika Knesset, uliolenga kupiga marufuku ziara za Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kwa wafungwa wa Kipalestina, haukupata kura za kutosha na haukupitishwa katika kikao hicho.
Kuanguka kwa muswada huo katika Knesset kulitokana na vyama vya Haredi (Wayahudi wa Kihafidhina) kususia kikao hicho, ikiwa ni maandamano dhidi ya sheria ya kuwataka vijana wao kujiunga na jeshi kwa lazima.
Gazeti la Kizayuni la Israel Hayom pia liliripoti kuwa Knesset imekataa rasimu ya sheria iliyolenga kuzuia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) kuwatembelea wafungwa wa Kipalestina.
Katika hatua ya kwanza ya upigaji kura, muswada huo ulipata kura 36 za kuunga mkono dhidi ya kura 41 za kuupinga, na kutokana na vyama vya Haredi kususia upigaji kura, haukufaulu kupata idadi ya kura zilizohitajika ili kupitishwa.