
New Jersey, Marekani. Timu ya taifa ya Ufaransa imekata tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Sweden, huku nyota wa kikosi hicho, Kylian Mbappe akiendelea kung’ara.
Katika mechi hiyo ya hatua ya 32 Bora iliyopigwa kwenye Uwanja wa MetLife, East Rutherford, New Jersey, Marekani, ilianza kuonekana mapema ya upande mmoja kutokana na Ufaransa kumiliki zaidi mpira kipindi cha kwanza tofauti na washindani wao wao, Sweden.
Ufaransa ilipata bao la kwanza dakika ya 45, kabla ya kwenda mapumziko kupitia Mbappe aliyemalizia pasi ya Ousmane Dembele na kuamsha shangwe zaidi kwa kikosi hicho.
Bao hilo lingekuwa la pili kwa Mbappe katika mechi hiyo baada ya dakika ya 21, kufunga pia, ingawa lilikataliwa na Mwamuzi Msaidizi wa Video (VAR), kutokana na nyota huyo alikuwa tayari ameotea.
Wakati Sweden ikiwa katika harakati za kusawazisha, dakika ya 53, Bradley Barcola akaifungia Ufaransa bao la pili akitumia vyema pasi ya Michael Olise na kuweka matumaini ya timu hiyo kusonga hatua inayofuata ya 16 bora.
Hata hivyo, matumaini ya Sweden ya kusonga mbele yalizidi kufifia baada ya Mbappe kuifungia Ufaransa bao la tatu dakika ya 74, akimalizia vyema pasi ya Olise.
Mbappe kwa sasa amefikisha mabao 18 katika Kombe la Dunia, akimzidi mawili aliyekuwa nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani, Miroslav Klose aliyefunga 16, huku akishika nafasi ya pili nyuma ya Lionel Messi wa Argentina mwenye 19.
Matokeo hayo yanaifanya Ufaransa kufuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia na itakutana dhidi ya Paraguay iliyofuzu kwa kuitoa Ujerumani kwa penalti 4-3, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 120.
Mechi hiyo kali na ya kusisimua zaidi inayosubiriwa kwa hamu kubwa ya hatua ya 16 bora na mashabiki wa soka, itachezwa Jumapili ya Julai 5, 2026, kwenye Uwanja wa Philadelphia.
Ufaransa ni miongoni mwa timu bora duniani zenye mafanikio makubwa katika Kombe la Dunia, ambapo imetwaa taji hilo mara mbili, ikianza na mwaka 1998, ilipokuwa mwenyeji wa fainali hizo baada ya kuichapa Brazil kwa mabao 3-0, Julai 12, 1998.
Timu hiyo ikachukua tena Kombe la Dunia mwaka 2018, fainali zilizofanyika Urusi baada ya kuifunga Croatia mabao 4-2, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Julai 15, 2018.
Pia, timu hiyo ilifika fainali mbili na kupoteza zote ikianza na ya mwaka 2006, ilipochapwa kwa penalti 5-3 dhidi ya Italia baada ya sare ya bao 1-1, kisha mwaka 2022, ikachapwa na Argentina kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya mabao 3-3, katika dakika 120.
Katika fainali ya mwaka 2006, iliyofanyika Ujerumani, Julai 9, 2006, moja ya tukio kubwa la kukumbukwa ni aliyekuwa mchezaji nyota wa Ufaransa na nahodha, Zinedine Zidane kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga kwa kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi.
Kwa upande wa Sweden imeshiriki Kombe la Dunia 2026 mara ya 13, tangu ilipoanza mwaka 1934, 1938, 1950, 1958, 1970, 1974, 1978, 1990, 1994, 2002, 2006, 2018 na sasa 2026, ikiwa ni miongoni mwa timu zenye rekodi ya kuvutia barani Ulaya.
Mafanikio makubwa kwa Sweden ni kufika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1958, ikiwa ndio mwenyeji, ambapo kikosi hicho kilikosa ubingwa baada ya kuchapwa na Brazil mabao 5-2, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Rasunda, Juni 29, 1958.
Pia, Sweden ni miongoni mwa timu zilizomaliza nafasi ya tatu mara mbili ambapo ilianza mwaka 1950, katika fainali hizo zilizofanyika Brazil, kisha ikarudia mwaka 1994, kwenye michuano hiyo iliyofanyika Marekani kama ilivyokuwa pia sasa.