
Mahakama ya Zanzibar inaendelea kuboresha utoaji wa huduma zake kupitia matumizi ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa haki.
Maboresho hayo ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (Electronic Case Management System eCMS) utakaonza kutumika rasmi katika Mahakama za kawaida na Mahakama za Kadhi kuanzia leo.
Usimamizi wa mashauri unajumuisha ufunguaji wa kesi, usajili, usikilizwaji na utoaji wa uamuzi wa Mahakama.
Ili kuhakikisha mabadiliko ya kutoka analogia kwenda kidigitali yanafanyika kwa ubora na ufanisi mkubwa mfumo huo kwa mujibu wa Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, utaanza kutumika kwa awamu tatu.
Awamu ya kwanza itaanza Julai mosi, 2026 na itahusisha Mahakama Kuu Masjala Kuu Tunguu pamoja na Divisheni zake, Mahakama ya Kadhi wa Rufaa Tunguu na Mahakama zote zilizopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Awamu ya pili itaanza Agosti mosi, 2026 na itahusisha Mahakama zote zilizopo Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Mkoa wa Kusini Unguja huku awamu ya tatu itaanza Septemba mosi, 2026 na itahusisha Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Pemba, Mahakama ya Kadhi wa Rufaa Pemba, pamoja na Mahakama zote zilizopo Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mkoa wa Kusini Pemba.
Kwa mujibu wa uongozi wa Mahakama, mashauri yatakayoanza kufunguliwa na kusikilizwa katika mfumo wa kielektroniki kwa kipindi hicho kilichotajwa kwa Mahakama husika, yatakuwa ni mashauri mapya tu.
Kwa mashauri yaliyofunguliwa kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo yaani kabla ya Julai mosi (leo) kurudi nyuma, yataendelea kusikilizwa kwa utaratibu wa zamani.
Wakati wa usikilizaji wa awali (PH0 katika mashauri ya jinai, mwenendo uliochukuliwa kielektroniki utaprintiwa na kusainiwa na wahusika na kisha kumbukumbu hizo zitaskaniwa na kupandishwa kwenye mfumo.
Rufaa au maombi yanayotokana na mashauri ambayo hayakufunguliwa na kusikilizwa kwa njia ya kielektroniki yataendelea kusikilizwa kwa njia ya zamani na kumbukumbu zote zitakazowasilishwa na kuhifadhiwa katika mfumo wa e-CMS zitachukuliwa kuwa ni kumbukumbu rasmi za Mahakama na zitatumika kwa madhumuni ya kiutawala na kimahakama kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na ugeni wa jambo lenyewe, kutakuwa na madawati ya usaidizi katika kila Mahakama ili kuwasaidia wananchi wasioweza kutumia mfumo na kipindi ambacho mfumo utakuwa umeanza kutumika katika Mahakama husika, hakuna shauri litakalokubaliwa kufunguliwa na kusikilizwa kwa njia ya zamani isipokuwa kwa muongozo wa Jaji Mkuu.
Licha ya muongozo huo kuanza kutumika mara tu ya kusainiwa na Jaji Mkuu, unaweza kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara kwa mujibu wa mahitaji katika kipindi cha matumizi ya mfumo.
Kwanza niipongeze mahakama katika hatua hizi kuhakikisha haibaki nyuma katika mabadiliko ya kidijitali yanaokwenda kwa kasi ulimwenguni kote, maana kwasasa kila kitu kinatumia teknolojia na kuachana na mifumo ya kizamani ya makaratasi.
Hata hivyo, ni vyema mkahakikisha mfumo unafanya kazi vizuri, tumekua tukishuhudia baadhi ya huduma zinazotumia mifumo kuleta usumbufu katika taasisi tofauti, mara mfumo umegoma, mara mfumo uko chini, mara mtandao umeruka na mambo mengine kama hayo.
Lengo la mifumo ni kuondosha changamoto lakini inaumiza pale inapoongeza badala ya kupunguza au kumaliza kabisa matatizo.
Sasa Mahakama ijitahidi sana mfumo uwe bora zaidi ili mambo yaende kwa kasi katika taasisi hii ya utoaji haki na kuongeza ufanisi jambo litakalochangia kuongeza imani kwa wananchi na wadau wote wanaotumia chombo hicho.
Pia, mahakama inapaswa ijikite zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya mfumo huo mpya wa kielektroniki ili wasiachwe nyuma na wawe tayari kukabiliana na mabadiliko yoyote yanayofanyika kwa maslahi mapana ya ustawi wa jamii.
Aidha katika kanuni namba 9 ni vyema Mahakama ikawa na ufuatiliaji wa karibu wa madawati hayo ili kutoruhusu kutoa mwanya wa kuibuka vishoka kwani uzoefu unaonesha katika sehemu za huduma huwepo watu wasio waaminifu kusubiri wale wasio na uelewa katika kupatiwa huduma husika kutaka kuwasaidia kwa kuchukua (fedha) ambazo zipo nje ya utaratibu wa kawaida jambo ambalo ni hatari pia.
Iwapo mambo haya yakizingatiwa kwa umuhimu wake, ni wazi kwamba tutashuhudia mabadiliko makubwa katika chombo hiki cha utoaji haki kwani itapunguza gharama zisizo na sababu, muda kwani haitakuwa tena lazima mtu kufika kwenye viunga vya mahakama badala yake atatumia mifumo katika uendeshaji wa kesi.
Kadhalika majaji na mahakimu wanaweza kusikiliza kesi popote wanapokuwa tofauti na kutakiwa kuwa ndani ya jengo la mahakama wakati wa kesi husika.