Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiwekea pingamizi Jamhuri katika maombi ya mapitio iliyowasilisha Mahakama ya Rufani, akidai hayana msingi wa kisheria kwa sababu yanapinga uamuzi ambao hauwezi kukatiwa rufaa wala kufanyiwa mapitio.
Kutokana na pingamizi hilo, Mahakama ya Rufani imeamua kusikiliza kwa pamoja hoja za pingamizi na maombi ya msingi ya Jamhuri, ikianza na pingamizi kabla ya kuamua shauri lote.
Jamhuri ilifungua maombi hayo Februari 24, 2026, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, uliokataa ombi lake la kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.
Shauri la mapitio namba 7203216/2026 limetajwa leo, Ijumaa Julai 3, 2026, mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani linaloongozwa na Jaji Augustine Mwarija, likiwajumuisha pia majaji Zainabu Muruke na Amour Khamis.
Badala ya kusikiliza pingamizi pekee na kuahirisha uamuzi wa maombi ya msingi, Mahakama imeelekeza hoja zote zisikilizwe pamoja.
Hii ina maana kuwa endapo itakubaliana na pingamizi la Lissu, haitakuwa na sababu ya kuamua maombi ya Jamhuri. Iwapo pingamizi litakataliwa, ndipo Mahakama itaendelea kutoa uamuzi kuhusu maombi ya msingi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akiwa katika kizimba cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam/
Hata hivyo, katika pingamizi lake, Lissu amedai kuwa maombi ya Jamhuri hayapo ndani ya mamlaka ya Mahakama ya Rufani kwa sababu yanalenga uamuzi wa muda, ambao haukuhitimisha kesi ya msingi.
Akinukuu uamuzi mbalimbali wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Lissu amesema ni msimamo wa mahakama hizo kuwa uamuzi unaoweza kukatiwa rufaa au kufanyiwa mapitio ni ule unaohitimisha haki za pande zote katika shauri.
Jopo la mawakili likiwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Lissu, uamuzi unaopingwa na Jamhuri haukumaliza kesi ya uhaini, bali ulikataa notisi ya kuwasilisha ushahidi wa nyongeza, huku kesi ya msingi ikiendelea kama kawaida.
Amesema hata maombi ya Jamhuri yanaonyesha wazi kuwa yanalalamikia kukataliwa kwa notisi ya kuwasilisha ushahidi mpya, jambo linalodhihirisha kuwa hayahusu uamuzi wa mwisho katika shauri.
Pia amedai kuwa Jamhuri haina mamlaka ya kuiomba Mahakama ifanye mapitio ya mwenendo wa shauri katika mazingira hayo, kwa kuwa mamlaka hayo ni ya Mahakama yenyewe.
Kilichotokea Mahakama Kuu
Chanzo cha mgogoro huo ni uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Februari 24, 2026 baada ya Jamhuri kuomba iruhusiwe kuwasilisha ushahidi wa nyongeza chini ya kifungu cha 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Upande wa mashtaka, kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliieleza Mahakama kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha notisi ya kuongeza ushahidi katika ushahidi wa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Amin Mahamba.
Katuga amesema ushahidi huo haukusomwa wakati wa mwenendo wa ukabidhi, uliofanyika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Alieleza kuwa Mahamba alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi, kwamba ushahidi huo ulibainika Februari 16, 2026 walipokuwa wakimuandaa shahidi huyo.
Lakini Lissu alipinga maombi hayo akisema kifungu cha 308(1) cha CPA kinahusu ushahidi uliokuwapo wakati wa mwenendo wa ukabidhi lakini haukusomwa, si ushahidi uliopatikana baadaye.
Amesisitiza kuwa ushahidi wa ACP Mahamba tayari ulikuwa umesomwa katika mwenendo wa ukabidhi, hivyo kuwasilisha ushahidi mwingine mpya chini ya shahidi huyo kungekuwa sawa na kubadili hati ya mashtaka.
Aidha, alisema kosa analokabiliwa nalo linadaiwa kutendeka Aprili 3, 2025 na alifikishwa mahakamani Aprili 10, 2025, ilhali ushahidi mpya unaotafutwa unahusu matukio yaliyotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika uamuzi wake, Jaji Dunstan Ndunguru alikubaliana na hoja za Lissu kuwa kifungu cha 308 cha CPA kinaruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi uliokuwepo wakati wa mwenendo wa ukabidhi lakini haukusomwa na si ushahidi uliopatikana baada ya hatua hiyo.
Jaji Ndunguru alisema notisi ya Jamhuri ililenga kuwasilisha ushahidi uliopatikana baada ya mwenendo wa ukabidhi na baada ya uchaguzi, hivyo haukuwepo wakati hatua hiyo ilipofanyika.
Kwa msingi huo, Mahakama iliikataa notisi hiyo, hatua iliyosababisha Jamhuri kufungua maombi ya mapitio katika Mahakama ya Rufani.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini, kinyume cha kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na kauli alizodaiwa kuzitoa kuhusu azma ya kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.