
Dar es Salaam. Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) unatarajia kusaini mikataba minane ya kwanza ya mikopo kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini, kwa lengo la kuboresha usalama wa biashara hiyo na kuongeza upatikanaji wa mafuta yanayokidhi viwango.
Mpango huo unaotekelezwa kupitia mikopo yenye masharti nafuu, na tayari umepokea maombi 150 kutoka maeneo mbalimbali nchini, jambo linaloonyesha mahitaji makubwa ya miundombinu salama ya biashara ya mafuta katika vijiji na miji midogo.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Julai 3, 2026, Mhandisi Mwandamizi wa Rea, Deusdedit Malulu amesema maandalizi ya kusaini mikopo ya kwanza yamekamilika, huku uchambuzi wa maombi mengine ukiendelea.
“Tunatarajia kusaini mikopo minane mwezi huu. Hii ndiyo hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi, lakini safari ndiyo inaanza. Kadri tunavyopata uzoefu, tutaendelea kutoa mikopo zaidi kwa waombaji watakaokidhi vigezo,” amesema.
Malulu amesema mpango huo ulianzishwa baada ya Rea kubaini ongezeko kubwa la matumizi ya vyombo vinavyotumia mafuta, zikiwamo pikipiki, maguta na magari katika maeneo ya vijijini, wakati biashara ya mafuta ikiendelea kufanyika katika mazingira yasiyo salama.
Amesema katika maeneo mengi mafuta bado huuzwa kwa kutumia chupa na vyombo visivyo rasmi, huku kiasi kinachobaki kikihifadhiwa ndani ya nyumba za wafanyabiashara, hali inayoongeza hatari ya moto na kuhatarisha maisha pamoja na mali za wananchi.
Mbali na changamoto za usalama, amesema Rea ilipokea malalamiko kuhusu ubora wa mafuta yanayouzwa kupitia mfumo huo usio rasmi, baadhi ya watumiaji waliripoti kuharibika kwa injini za vyombo vyao kutokana na mafuta yasiyo bora.
“Kutokana na hali hiyo tuliona kuna haja ya kuja na suluhisho linaloendana na mazingira ya vijijini. Tulihitaji mradi wenye gharama nafuu lakini unaowezesha ujenzi wa vituo salama vya mafuta vinavyokidhi viwango,” amesema.
Amesema kiwango cha mkopo cha hadi Sh133 milioni kilibainishwa baada ya mashauriano kati ya REA, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) pamoja na Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Tapsoa).
“Kiasi hiki kilibainika kuwa kinatosha kujenga kituo cha mafuta kinachokidhi mahitaji ya maeneo ya vijijini,” amesema.
Kwa mujibu wa Malulu, ili kuwavutia wawekezaji wadogo, mkopo huo unatolewa kwa riba ya asilimia tano kwa mwaka na muda wa marejesho wa hadi miaka saba.
Amesema Rea pia imeondoa moja ya changamoto kubwa zilizokuwa zinawakwamisha wananchi wengi kupata mikopo kwa kuruhusu waombaji wasiokuwa na dhamana za kawaida, kutumia kituo cha mafuta kitakachojengwa kama sehemu ya dhamana ya mkopo.
“Tumefanya hivyo ili kuwapa nafasi wananchi wengi zaidi kunufaika na mpango huu,” amesema.
Hata hivyo, amesema waombaji wanatakiwa kumiliki eneo lenye hati halali, iwe hatimiliki au hati ya kimila, na eneo hilo liwe katika kijiji au mji mdogo, badala ya maeneo yaliyopo kandokando ya barabara kuu zinazounganisha mikoa.
“Lengo letu ni kuwafikia wananchi wa vijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma hizi muhimu. Hatujalenga vituo vilivyopo kandokando ya barabara kuu, bali maeneo ambayo bado yana upungufu mkubwa wa huduma za mafuta,” amesema.
Akizungumzia mwenendo wa maombi, Malulu amesema yamepokewa kutoka karibu kila mkoa nchini, huku mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiongoza kwa mwitikio.
Amesema kati ya maombi 150 yaliyowasilishwa, mengi yalihitaji kufanyiwa uchambuzi zaidi kwa kuwa baadhi ya waombaji hawakuwa wameelewa kikamilifu utaratibu na vigezo vya mpango huo.
“Ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu kupitia warsha na makongamano ili wananchi waelewe masharti ya mradi na namna sahihi ya kuwasilisha maombi,” amesema.
Amewataka wananchi wanaotaka kunufaika na mpango huo kutembelea tovuti ya REA, kusoma mwongozo wa maombi kwa makini na kuhakikisha wanatimiza vigezo vyote kabla ya kujaza na kuwasilisha fomu.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda la REA katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), Linus Vutalis amesema pamoja na utoaji wa mikopo, kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanaouza mafuta kwa kutumia chupa kuhusu namna ya kujikinga na ajali za moto.
“Si wote watakaoweza kupata mikopo hii. Ni muhimu wale wanaoendelea na biashara hiyo wapatiwe elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza. Hilo halimaanishi kuhalalisha biashara katika mazingira hayo, bali kupunguza hatari zinazoweza kutokea, ikiwamo kuhifadhi mafuta ndani ya nyumba,” amesema.