
Dar es Salaam. Zaidi ya watu 100 waliokuwa wakishiriki maandamano ya kupinga muungano wa kijeshi wa Nato, wamekamatwa nchini Uturuki, siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano wake wa kilele mjini Ankara.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Deutsche Welle (DW), operesheni hiyo ya kukamata ililenga waandamanaji waliokuwa wameandaliwa na chama cha kisiasa cha mrengo wa kushoto nchini Uturuki (TKP), kinachopinga ushawishi wa Nato na sera za kijeshi za nchi za Magharibi.
DW imeripoti TKP ilitoa taarifa ikieleza zaidi ya wanachama wake 100, wakiwemo waratibu wa maandamano, walikamatwa kabla ya kufanyika kwa mkusanyiko uliopangwa katika eneo la Kizilay, katikati ya mji wa Ankara.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikutoa maelezo ya kina kutoka upande wa serikali ya Uturuki kuhusu sababu mahsusi za kukamata watu hao, zaidi ya hatua za jumla za kiusalama zilizokuwa zimewekwa.
Mamlaka za Uturuki zimeimarisha ulinzi mkali katika mji mkuu Ankara, zikijumuisha kufungwa kwa baadhi ya barabara, kuwekwa kwa vizuizi vya usalama, na kupigwa marufuku kwa mikusanyiko isiyoidhinishwa katika maeneo kadhaa ya jiji.
Hatua hizi zinatajwa kuwa sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kilele wa Nato unaotarajiwa kuanza kesho Jumanne Julai 7,2026, ukiwakutanisha viongozi kutoka nchi 32 wanachama pamoja na maofisa wa ngazi za juu wa muungano huo wa kijeshi.
Kuhusu Nato
Nato ni muungano wa kijeshi ulioanzishwa mwaka 1949 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa lengo la ulinzi wa pamoja kati ya mataifa ya Ulaya na Amerika Kaskazini, wenye makao yake makuu Brussels, Ubelgiji.
Muungano huo unafanya kazi kwa msingi wa ulinzi wa pamoja, ambapo shambulio dhidi ya nchi mwanachama mmoja huchukuliwa kama shambulio dhidi ya wote kupitia kifungu cha tano cha mkataba wake.
Kazi zake kuu ni kulinda usalama wa wanachama, kuzuia migogoro, kupambana na ugaidi na kuratibu ushirikiano wa kijeshi.
Kwa sasa Nato ina jumla ya nchi 32 wanachama, zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uturuki yenyewe.
Tanzania si mwanachama wa Nato na haijawahi kuwa mwanachama tangu kuanzishwa kwa muungano huo, kwani inafuata sera ya kutofungamana na upande wowote katika masuala ya kijeshi ya kimataifa.
Mkutano wa kilele wa Nato unaotarajiwa kufanyika Ankara unalenga kujadili masuala ya usalama wa kimataifa, migogoro ya kikanda, ulinzi wa pamoja, usalama wa mtandao na uimarishaji wa bajeti za ulinzi miongoni mwa nchi wanachama.
Hata hivyo, maandamano yaliyoandaliwa na TKP yanaonesha kuwepo kwa upinzani wa ndani dhidi ya Nato nchini Uturuki, ambapo baadhi ya makundi ya kisiasa ya mrengo wa kushoto yanaiona jumuiya hiyo kama chombo cha ushawishi wa kijeshi wa mataifa makubwa duniani.
Hali hiyo imeongeza mjadala kuhusu nafasi ya Nato katika siasa za kimataifa, hasa wakati wa mkutano huu wa kilele ambapo dunia inakabiliwa na misukosuko ya vita na mapigano maeneo mbalimbali ikiwemo Mashariki ya Kati.