
Kigoma. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, imeanza kupokea ushahidi wa walalamikaji katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo.
Baba Levo alitangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hata hivyo, wananchi wanne, Johary Kabourou, Lumu Hamis Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali, wamefungua kesi dhidi ya INEC, mbunge huyo Chipando na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakipinga uchaguzi huo.
Katika kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, wadai hao, ambao wanajitambulisha kuwa wapiga kura katika jimbo hilo, wanadai uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi.
Wanabainisha kasoro hizo ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyoonyeshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Hivyo, wanaiomba mahakama hiyo, pamoja na mambo mengine, iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.
Shahidi wa kwanza
Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani na kufungua pazia la ushahidi huo leo Jumatatu, Julai 6, 2026, ni Lumu Hamis Mwitu ambaye ni mmoja wa walalamikaji katika kesi hiyo.
Akiongozwa na wakili wa walalamikaji, shahidi huyo ameiomba mahakama iupokee ushahidi wake wa maandishi ambao alikwisha kuuwasilisha mahakamani.
Nyaraka hiyo imepingwa na mawakili wa walalamikiwa, akiwemo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, ambaye ameiomba mahakama isiyapokee maelezo hayo, pamoja na mambo mengine, akidai si nyaraka halisi na kwamba haijawahi kuwafikia wao.
Pingamizi hilo limeungwa mkono pia na wakili wa Baba Levo, Daniel Rumenyela, kwa hoja hizo hizo.
Akijibu hoja hizo, wakili wa walalamikaji, John Seka, amepinga hoja za mapingamizi ya walalamikiwa, pamoja na mambo mengine, akidai mahakamani hapo ziliwasilishwa nyaraka mbili zinazomhusu shahidi huyo.
Nyaraka hizo ni pamoja na maelezo yake pamoja na nyaraka inayoonyesha viungo (link) mbalimbali vya picha jongefu (video) katika mitandao, na kwamba nyaraka hiyo ilishawasilishwa mahakamani tangu Juni 15, 2026, siku ya usikilizwaji wa awali.
Wakili Seka amesisitiza maelezo hayo tayari yako katika mfumo wa mahakama.
Pia amedai nyaraka hiyo ni halisi na imesainiwa na shahidi huyo kwa mkono wake, hivyo hakuna namna ambayo inaweza kuwa nakala kivuli.
Vilevile, wakili Seka ameieleza mahakama kuwa shahidi huyo ameweka msingi wa upokeaji wa nyaraka hiyo, pamoja na mambo mengine, kwa kuitambua kuwa ina jina na saini yake.
Ingawa mawakili wa walalamikiwa katika majibu yao dhidi ya hoja za wakili Seka walisisitiza ni nakala kivuli, Jaji Victoria Nongwa katika uamuzi wake amekubaliana na hoja za wakili Seka na kutupilia mbali pingamizi la walalamikiwa.
Baada ya uamuzi huo, shahidi huyo, akiongozwa na wakili Seka, ameiomba mahakama iyapokee maelezo yake hayo na mahakama imeyapokea.
Baada ya maelezo hayo kupokewa, ambayo mawakili wa walalamikiwa wamesema wameshayasoma, mawakili hao wameanza kumhoji maswali mbalimbali ya dodoso kuhusiana na yale aliyoyaeleza katika maelezo yake hayo.
Pamoja na mambo mengine, shahidi huyo katika maelezo yake hayo ameeleza kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi huo alifanya upelelezi na kukusanya ushahidi kuhusu masuala ya rushwa na alikuwa akipeleka taarifa hizo kwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Abdul Nondo.
Hivyo ameieleza mahakama kuwa amekuja kuieleza kuhusu masuala ya rushwa na takrima.
‘Rushwa ya Sh100,000’
Pia ameeleza kuwa wakati kampeni zinaendelea alimuona Baba Levo akiongozana na kundi la watu katika harusi moja ambapo alitoa Sh100,000 akidai ni mchango wake kwa ajili ya harusi hiyo, lakini hapo hapo akamuomba kura bibi harusi.
Hata hivyo, alipoulizwa na wakili Kalokola kama kutoa mchango katika harusi ni rushwa, amejibu kuwa kutoa mchango kwa ajili ya harusi si rushwa, lakini mchango hautolewi siku ya harusi na kuomba kura.
Alipoulizwa iwapo ana utaalamu wa uchunguzi wa masuala ya rushwa, amejibu hana na kwamba anaifahamu TAKUKURU kuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, lakini akasema si yeye wala Zitto Kabwe au Abdul Nondo aliyewahi kupeleka taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU dhidi ya Baba Levo.
Pia amekiri kuwa hajawahi kusikia kuwa Baba Levo amewahi kushtakiwa katika mahakama yoyote kuhusiana na vitendo vya rushwa wala kuhojiwa na TAKUKURU.
Vilevile, amekiri taarifa alizoziandika katika maelezo yake hayo ni taarifa ambazo nyingine hakuzishuhudia, bali ni maelezo aliyoyasikia kutoka kwa watu wengine.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, George Kalenda, shahidi huyo amejibu hawakuwahi kuripoti Takukuru vitendo vya rushwa dhidi ya Baba Levo kwa kuwa taarifa hizo zilikuwa wazi katika mitandao ya kijamii na Takukuru walikuwa wanaziona.
“Sasa kama wao (Takukuru) hawakumkamata, sasa sisi tungefanye nini?” amehoji shahidi huyo.
Akihojiwa na wakili Rumenyela anayemwakilisha Baba Levo, amesema alipoulizwa ni mwanachama wa chama gani alijibu yeye ni mpiga kura wa Jimbo la Kigoma Mjini na kwamba wakati wa kampeni alikuwa kwenye timu ya mgombea wa ACT-Wazalendo ambaye alimuomba kibinafsi.
Ameeleza jukumu lake katika kampeni hizo lilikuwa kwenye timu ya maudhui ya mgombea huyo, lakini akajibu kuwa si mtaalamu wa maudhui.
Shahidi huyo ameeleza kuwa kwenye kamati hiyo walikuwa wakifuatilia sera za wagombea wengine kuona kama wana chochote, na kwamba walipowafuatilia walikuta hawana sera bali waliwakuta wakigawa rushwa.
Akisoma maelezo yake, amefafanua kuwa katika mkutano mmoja wa kufunga kampeni Baba Levo alimuita mwanakamati mwenzao na kumtambulisha msanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva), Diamond Platnumz (Naseeb Abdul), kwamba ni msanii anayependwa sana, kisha akamruhusu kutoa fedha kwa waliohudhuria mkutano huo.
Pia, amesema katika mkutano mwingine Baba Levo akiwa na viongozi wa CCM walikuwa wakigawa nguo kama fulana, khanga na kofia.
Lakini alipoulizwa kama ni kosa kwa mgombea kuwagawia watu wake nguo kama sare za chama chake na mabango ili kufanikisha shughuli yake, amesema siyo tatizo kugawa sare za chama.
“Alikuwa anagawa khanga anasema, ‘Chukua na hii umpelekee mkeo nyumbani akipigie Chama Cha Mapinduzi,'” amesema shahidi huyo.
Kuhusu mchango alioutoa Baba Levo harusini, amesema siku hiyo Baba Levo na watu wake walikuwa kwenye kampeni ya nyumba kwa nyumba, akafika kwenye nyumba moja iliyokuwa na harusi, akatoa Sh100,000 akampa bibi harusi kisha akamuomba kura, jambo ambalo yeye alilitafsiri kuwa ni rushwa.
Akihojiwa na Wakili Seka katika maswali ya kusawazisha majibu ya maswali ya walalamikiwa, shahidi huyo amefafanua kuwa mchango alioutoa Baba Levo harusini aliutafsiri kuwa ni rushwa kwani alitaka kujionyesha kwa jamii kuwa ni mtu mwema anayeweza kusaidia watu.
Pia amesema sheria hairuhusu mgombea kugawa nguo wakati wa kampeni.
Kesi hiyo itaendelea Jumatano, Julai 8, 2026, kwa mashahidi wengine.