Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7
Mmoja wa magwiji wakubwa wa soka atahitimisha taaluma yake bila kushinda taji muhimu zaidi, baada ya mechi ya mwisho ya Kombe la Dunia ya Cristiano Ronaldo akiwa na Ureno kumalizika kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Uhispania katika hatua ya 16 bora.
Mchezaji huyo alibubujikwa na machozi wakati safari yake ya Kombe la Dunia ilipofikia tamati, kufuatia bao la ushindi lililofungwa na Mikel Merino katika muda wa nyongeza, bao lililoiwezesha timu ya nchi jirani kusonga mbele.
Akiwa na umri wa miaka 41, mchezaji huyo ambaye ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara tano, Ligi ya Mabingwa mara tano na Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro) mwaka 2016, amefunga mabao 976 —rekodi ya dunia— akiwa na klabu zake pamoja na timu ya taifa.
Amefunga mabao katika mashindano sita ya Kombe la Dunia, rekodi ya kihistoria.
Hata hivyo, hatua ya karibu zaidi aliyofikia katika mbio zake a kushinda Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 2006, wakati Ureno ilipotinga nusu fainali.
Tayari alikuwa ametangaza kuwa hili lingekuwa Kombe lake la Dunia la mwisho, lakini baada ya mechi hiyo alisema: “Nitajadiliana na familia yangu na kufanya maamuzi kwa utulivu,” alipoulizwa iwapo ataendelea kuichezea timu yake ya taifa.
Mjadala utaendelea kuwa wazi laitiUreno wangekuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushinda Kombe hili la Dunia bila shinikizo la kumwanzisha Ronaldo – mchezaji wa klabu ya Al-Nassr – katika kila mechi.
Hata hivyo, kwa mchambuzi wa BBC Chris Sutton, ambaye alikuwa kwenye mchezo huo mjini Dallas, hakukuwa na shaka.
“Anazunguka uwanja kwa shida, kama mzee; ndiyo maana Ureno haipo,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Uingereza.
“Cristiano Ronaldo hafanyi chochote; hakufanya lolote.”
“Roberto Martínez anafanya nini? Unawezaje kumfurahisha mchezaji kiasi hiki?”
“Ureno imetupwa nje kwa sababu ya Roberto Martínez.”
Kocha Martinez alitangaza kujiuzulu baada ya firimbi ya mwisho na kumsifu Ronaldo, ambaye alimwita “nyota wa soka”.
“Tunapaswa kumshukuru kwa kile alichojaribu kufanya katika Kombe hili la Dunia,” Martinez alisema.
“Ndoto yake ilikuwa kushinda Kombe hili la Dunia, na alikabiliana nayo kwa kutoa mfano wa ajabu.”
“Yeye ni mfano mzuri wa kile soka inawakilisha na ubora wa binadamu kwenye ulingo wa mwanariadha.”
Je, Ronaldo alifaa kucheza?
Chanzo cha picha, Getty Images
Suala kuu linalojirudia mara kwa mara katika mashindano makubwa ya hivi karibuni ni iwapo Ronaldo anapaswa kuwa mmoja wa wachezaji wanaoanza mechi.
Amefunga mabao 146 kwa timu yake ya taifa, rekodi katika soka la kimataifa la wanaume, lakini hivi karibuni baadhi ya watu wamehoji iwapo bado ana mchango mkubwa uwanjani.
Na, kutokana na umaarufu na hadhi yake inayovuka mipaka ya michezo, inaonekana Martinez hakuthubutu kumuacha nje ya kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, timu hiyo iliyo na baadhi ya mabeki na viungo bora duniani labda ilitarajia kufikia mafanikio makubwa zaidi ya hatua ya 16 bora.
Wachezaji wanne wa kikosi hicho walisaidia Paris Saint-Germain kushinda mataji mawili ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya: beki wa kushoto Nuno Mendes, viungo Vitinha na João Neves, na mshambuliaji Gonçalo Ramos (aliyejiunga na AC Milan msimu huu wa joto).
Bruno Fernandes, wa Manchester United, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu ya England (EPL).
“Unamuacha vipi Gonçalo Ramos nje ya uwanja?” Sutton alihoji.
“Ni aibu kubwa kwa kocha; alikubali tu matakwa ya mchezaji wake nyota.”
“Yeye ndiye mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi kuwahi kutokea Ureno, lakini unahitaji sifa zaidi ya hizo.”
Ronaldo alimaliza mashindano hayo akiwa na mabao matatu: mawili dhidi ya Uzbekistan na bao moja la penalti dhidi ya Croatia.
Lakini, licha ya kuwepo kwa wachezaji 10 waliofunga mabao mengi zaidi, ni wachezaji wanne pekee waliofanya majaribio mengi zaidi ya mashuti kuliko Ronaldo, ambaye alipiga mashuti 18.
Ronaldo alifikisha idadi sawa ya majaribio na Mnorwe Erling Haaland, ambaye kwa sasa anashiriki nafasi ya ufungaji bora akiwa na mabao 7.
Kwa upande mwingine, alitengeneza nafasi moja tu ya kufunga bao kwa mchezaji mwenzake katika mechi zake zote tano.
Wachezaji wapatao 366 waligusa mpira mara nyingi zaidi kuliko Ronaldo wakati wa Kombe la Dunia, ingawa alicheza kila dakika ya mechi tano za Ureno, isipokuwa dakika tisa pekee.
Martínez alisema: “Unapohitaji bao, huwezi kumtoa Cristiano uwanjani, angalau si kwa dakika zote 90; ana uwezo wa kimwili. Uwepo wake, uchezaji wake katika nafasi zilizo wazi, kwa kweli… tunahitaji uzoefu wake.”
Je, hii ni hoja nyingine ya Messi katika mjadala wa “GOAT”?
Chanzo cha picha, Getty Images
Umaarufu wa Cristiano Ronaldo —mchezaji wa zamani wa Sporting, Manchester United, Real Madrid na Juventus— na mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi, umebadilisha kabisa jinsi watu wanavyofurahia na kufuatilia soka.
Wengi hujiona kuwa wafuasi wa Ronaldo au Messi —gwiji wa Barcelona na mshambuliaji wa zamani wa PSG— badala ya kuwa mashabiki wa klabu fulani.
Hakuna kundi lolote kati ya hayo mawili litakalokubali kubadili msimamo wake katika mjadala wa nani kati yao ni mchezaji bora zaidi wa muda wote, ikiwa kweli kuna mmoja anayestahili sifa hiyo.
Hata hivyo, hadi mwaka wa 2022, shutuma pekee iliyoelekezwa kwa wote wawili hao ilikuwa kwamba hawahakuwahi kushinda Kombe la Dunia, taji ambalo magwiji kama Pelé na Diego Maradona waliwahi kulinyanyua.
Messi aliongoza Argentina kulinyakua taji hilo mwaka wa 2022 nchini Qatar, na hivyo kuvuka kikwazo hicho. Kwa upande mwingine, Ronaldo atastaafu bila kulishinda taji hilo.
Ingawa wachezaji wote wawili wako katika hatua za mwisho za taaluma zao —Ronaldo akiwa Saudi Arabia na Messi akiwa Marekani na klabu ya Inter Miami—, hakuna shaka kwamba Messi anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika hatua hii.
Yeye ndiye anayeshikilia rekodi ya pamoja ya ufungaji bora katika Kombe la Dunia akiwa na mabao 8, akifikia idadi hiyo katika michuano hii sasa Ronaldo ana mabao manne katika michuano hiyo kwa ujumla.
Wayne Rooney, mchezaji mwenzake wa zamani wa Ronaldo katika klabu ya United, alisema: “Yeye ni gwiji, ni nyota mkubwa. Mchango wake katika soka na kwa mamilioni ya watu ni wa kipekee.”
“Bila shaka amevunjika moyo kwa sababu alikuwa na matumaini ya kushinda michuano hii. Lakini ndio hivyo tena. Ni siku ya huzuni kwa soka.”
“Lazima tutabasamu kwa sababu tulishuhudia akicheza”
Chanzo cha picha, Getty Images
Ronaldo bado anashikilia rekodi moja au mbili za Kombe la Dunia kutokana na muda mrefu aliocheza katika kiwango cha juu.
Yeye ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao katika mashindano sita ya Kombe la Dunia na mmoja kati ya wachezaji wawili pekee walioshiriki katika matoleo sita, akiwa pamoja na Messi.
Mabao yake 11 yanamweka katika nafasi ya tisa kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote, orodha inayoongozwa na Messi mwenye mabao 20.
Hata hivyo, bao moja tu kati ya hayo lilifungwa katika hatua ya mtoano: mkwaju wa penalti dhidi ya Croatia katika hatua ya 32-bora ya michuano hiyo.
Kwa kweli, Ronaldo aliwekwa benchi wakati wa hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia lililopita — ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2008 kutocheza mechi kuanzia dakika ya kwanza katika michuano mikubwa — kufuatia kutoelewana na kocha wa wakati huo, Fernando Santos.
Sutton, mshambuliaji wa zamani wa Blackburn, aliongeza: “Gonçalo Ramos alicheza katika hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia lililopita na kufunga mabao matatu (hat-trick) wakati kocha alipokuwa na ujasiri wa kumwacha Ronaldo nje ya kikosi.
“Miaka minne imepita, Ronaldo amezeeka kwa miaka minne, na tazama kilichotokea.”
Mashabiki wa Ureno waliozungumza na BBC baada ya mchezo huo walionyesha huzuni kwamba huu ulikuwa mwisho wa safari ya Ronaldo katika Kombe la Dunia.
Mmoja wao alisema: “Ndoto yangu mojawapo ilikuwa kumuona Ronaldo ana kwa ana. Nilifurahi kumuona. Ilikuwa na maana kubwa sana.”
“Nina msisimko mkubwa. Hatukuwa na bahati wakati huu. Kile alichokifanya Ronaldo kilikuwa kizuri. Hatupaswi kulia, tunapaswa kutabasamu kwa sababu tulimuona akicheza.”
“Hakuna sababu ya kuendelea”: Martínez aondoka Ureno
Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha wa zamani wa klabu za Swansea, Wigan na Everton, Roberto Martinez, aliiongoza timu ya taifa ya Ubelgiji kati ya mwaka 2016 na 2022 na timu ya taifa ya Ureno kuanzia mwaka 2023.
Kocha huyo raia wa Uhispania aliiongoza Ubelgiji kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018, ambapo walifungwa na Ufaransa, lakini baadaye waliondolewa katika hatua ya makundi mwaka 2022.
Ingawa alishinda taji la Nations League akiwa na Ureno mwaka jana, anaondoka katika wadhifa wake kufuatia kuondolewa kwa Ureno katika michuano hii ya Kombe la Dunia.
“Nilikuja Ureno nikiwa na lengo la kushinda Kombe la Dunia na, kwa kuwa nilishindwa kufanya hivyo, hakuna sababu ya kuendelea,” alisema.
“Mkataba wangu unaisha leo.”
Sutton aliongeza: “Kazi yake ilikuwa kujaribu kushinda Kombe la Dunia na kupanga kikosi bora zaidi kwa ajili ya Ureno.”
“Je, amefanikiwa? Hata kidogo.”
“Namna timu hii ilivyoendeshwa ni ya kusikitisha na aibu.”
“Aliharibu mradi wa Ubelgiji wakati walipokuwa na fursa ya kufikia mambo makubwa na kizazi hicho cha dhahabu; mwishowe wakawa kitu cha dhihaka katika soka.”
“Na kipindi hiki akiwa na Ureno… ilikuwa jambo la kusikitisha kuona kocha akifanya hivyo.”