
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ametia saini marekebisho ya katiba yanayoongeza muda wake wa kusalia madarakani hadi mwaka 2030.
Marekebisho hayo yanaongeza muda wa uongozi wa Rais na Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kuondoa mfumo wa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais, huku yakiruhusu rais kuchaguliwa na bunge.
Bunge la Zimbabwe lilipitisha marekebisho hayo mwezi uliopita baada ya chama tawala cha Zimbabwe Zanu-pf kupata wingi wa kura wa theluthi mbili unaohitajika katika mabunge yote mawili.
Nick Mangwana Msemaji wa serikali ya Zimbabwe amesema kuwa
Imesainiwa, imethibitishwa na kukabidhiwa rasmi – sasa ni sheria.
Mangwana ameeleza haya katika chapisho aliloweka kwenye mtandao wa X.
Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83 alipasa kuondoka madarakani mwaka 2028 lakini sasa atasalia madarakani hadi mwaka wa 2030.
Sheria hiyo ambayo inaondoa uchaguzi wa rais imepingwa na vyama vya upinzani nchini Zimbabwe.
Mwezi uliopita, mabunge yote mawili ya Zimbabwe yaliidhinisha muswada huo.
Dalili za Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 83, kusalia madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takribani miaka miwili iliyopita.
Mwaka jana chama cha Zanu-pf kilipitisha azimio lal kufanya marekebisho ya katiba ili kuongeza muda wa mihula ya urais. Pendekezo hilo liliidhinishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Februari mwaka huu.